Makala za maoni

MIKOPO NA MISAADA: MTEGO UNAOHITAJI MBINU KUUKWEPA

Na Abbas Mwalimu

Analyst: Strategist: Researcher| Politics| Security| Conflicts|International Relations| Diplomacy
Mtego katika mikopo au misaada ya kigeni huwa kwenye vigezo na masharti (terms and conditions) ya mkataba wa mkopo au msaada husika.
Vigezo na masharti ya mikopo au misaada husababisha nchi au taasisi kujikuta kwenye mtego wa madeni (debt trap).
Hali hiyo huifanya nchi au taasisi kuwa mtumwa wa madeni yake kwa nchi au taasisi inayoidai.
Lakini licha ya ukweli huo kuhusu mikopo na misaada, tishio hilo haliondoi ukweli kuwa kuna wakati ni lazima nchi ikope ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Lengo la nchi kukopa huja pale ambapo Serikali inahitaji kutekeleza miradi ya maendeleo na wakati huo ina ufinyu wa bajeti.
Kutokana na hali hiyo, Serikali hulazimika kukopa au kupokea misaada kwa ili kutekeleza miradi hiyo.
Hivyo, ukopaji ni lazima uzingatie miradi ambayo itaenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa mantiki hiyo, nchi hukopa pale penye ulazima wa kufanya hivyo na si kwa sababu ati kuna fursa ya kukopa.
Katika muktadha huo, mikopo au misaada haikwepeki. Ni kama katika maisha yetu ya kawaida tunavyokopa benki kwa ajili ya biashara.
Hali hii ipo pia kwa nchi. Hivyo basi, suala kubwa katika mikopo au misaada ni kuweza kubaini na kukwepa mitego inayowekwa katika mikopo au misaada hiyo.
Ili kuweza kufahamu mitego inayowekwa katika mikopo au misaada, ni vema tutumie mfano wa mkopo wa kutoka Shirika la Fedha Duniani ili kujenga uelewa wa pamoja.
Wakati mapambano dhidi ya Uviko-19 yaliposhika hatamu, Shirika la Fedha Duniani (International Monetary Fund-IMF) lilikuwa likitoa misaada na mikopo ya fedha kwa nchi mbalimbali duniani.
Muongozo wa fedha zile ulizitaka nchi kununua vipukusi (sanitizer), barakoa na chanjo. Huu ndiyo mtego uliokuwa katika mkopo huo.
Uzoefu unaonesha kuwa nchi kubwa duniani au mashirika na taasisi za fedha huweka vigezo na masharti ambayo nchi inayopokea mkopo au msaada ikiyafuata hujikuta kwenye mtego.
Kwa hiyo suala la msingi ni kukwepa mitego hiyo. Kadhalika jambo jingine muhimu ni kuhakikisha unabaki katika lengo lako la msingi. Lakini je unakwepaje mitego na unabaki vipi kwenye lengo?
Nickols (2011) alibainisha kwa kusema, ‘Strategy can fail and when it does, tactics dominate the action. Execution becomes strategy.’
Katika stratejia, kuna wakati mkakati hukwama. Mkakati unapokwama mbinu hutawala kitendo. Hivyo, utekelezaji hugeuka kuwa mkakati.
Hapa ndipo ambapo mtego huweza kukwepwa. Kadhalika, hapa ndipo Tanzania ilipokwepa mtego wa kununua sanitaiza, barakoa na chanjo katika mkopo wa Trilioni 1.3 ilizopokea kutoka IMF.
Mbinu mojawapo muhimu katika mkakati ni kupendekeza njia mbadala ambayo haitaathiri lengo.
Hivyo, katika hali ambayo IMF walielekeza pesa itumike kwa ajili ya kununua sanitaiza, mbadala wa sanitaiza ni maji. Hivyo Tanzania ilikwepa mtego huo na hatimaye kuzielekeza fedha zile kwenye uchimbaji wa visima.
Aidha, IMF walipoelekeza fedha zile zitumike kununua barakoa kwa sababu ya msongamano wa watu, mbadala wa barakoa ni kujenga madarasa mengi ili kupunguza msongamano wa watu/wanafunzi madarasani. Hapa Tanzania ilifanikiwa kukwepa mtego wa vigezo na masharti.
Halikadhalika, IMF walipoelekeza fedha zile zitumike kununua chanjo lakini Uviko-19 inafaa kuwahiwa ikiwa katika hatua za awali basi ujenzi wa vituo vya afya na hospitali ndiyo njia mbadala. Tanzania ikafanikiwa kukwepa mtego huo pia.
Kimkakati, ili kuweza kukwepa mtego wowote katika makubaliano ni lazima mkakati uwe na maeneo mawili ya msingi:
(i) Mkakati kama ulivyopangwa hapo awali kabla hamjaingia kwenye meza ya majadiliano
(ii) Mkakati kuweza kunyumbulika kulingana na mazingira yanayojitokeza katika chumba cha majadiliano na kuweza kukabiliana nayo.
Mambo hayo mawili huwezesha nchi au taasisi kukwepa mitego itakayoweka kwenye mikopo au misaada. Makubaliano ya IMF na Tanzania wakati ule yanasadifu mambo hayo.

Back to top button