Makala za maoni

????????????????????????????????????: ???????? ???????????????????????? ???????????????????? ???????? ?????????????????????????????

 Abbas Mwalimu 

Baada ya ushawishi na juhudi za dhati kwa zaidi ya miongo saba, tarehe 07 Julai imekuwa siku adhimu kwa Afrika na dunia kwa ujumla.

Hii ni siku ambayo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliitangaza siku hiyo kuwa Siku ya Kiswahili Duniani kila mwaka.

Kikao cha 41 cha Mkutano Mkuu wa UNESCO kilichoketi jijini Paris Novemba 2021, kiliamua kuitangaza siku hiyo kwa Azimio namba 41C/62 kwa kutambua mchango wa Kiswahili katika kukuza na kulinda utamaduni wa Mwafrika.

Ikumbukwe kuwa mnamo miaka ya 1950 Umoja wa Mataifa ulianzisha kitengo cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja huo.

Hilo halikuja bure, zipo sababu kadhaa zilizopelekea kuanzishwa kwa kitengo hicho.

Kipekee, siku hii imekuwa muhimu zaidi kwa Tanzania.

Umuhimu wa siku na tarehe hii kwa Tanzania unakuja katika sura mbili, mosi hii ni tarehe ambayo Tanzania husherekea kilele cha Maadhimisho ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Saba Saba.

Pili ni kwamba tarehe 07 Julai 1954, ni siku ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza rasmi kwamba ‘Kiswahili kitakuwa ndiyo nyenzo pekee na muhimu ya kufikia Uhuru.’

Aidha, kabla ya hatua hiyo ya UNESCO kutangaza tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, hatua kadhaa zilipitiwa.

Mnamo tarehe 11 Septemba 2017, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipitisha Azimio Namba 71/328 likielekeza kuwepo kwa siku Maalumu ya Kusheherekea lugha zake rasmi ili kuelezea historia na utamaduni wa lugha hizo.

Katika muktadha huo, Kiswahili kimechukuliwa kuwa ni lugha ya Afrika.

Kuwepo kwa siku hii ni mafanikio makubwa kwa Tanzania ingawa inaonekana bado hakujawa na mikakati thabiti ya kutumia fursa hiyo.

Kupitia Kiswahili Tanzania ina nafasi kubwa sana kupenyeza ushawishi wake barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Lakini hilo litawezekana endapo tu kutakuwa na mikakati thabiti ya kutumia Kiswahili kama nyenzo ya kufikia ajenda za kinchi.

Kadhalika, licha ya kutajwa kwenye Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania kama nyenzo ya diplomasia, lakini bado hakujawa na juhudi za dhati za kukuza Kiswahili.

Tanzania iliweza kuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika miaka ya 1960-1980 kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa nini ishindikane sasa?

Mafaniko ya Kiswahili yamepitia hatua mbalimbali ambazo hatuna budi kuzitambua kama nilivyogusia hapo awali.

Harakati mbalimbali zilifanyika na zinaendelea kufanyika ili kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano barani Afrika.

Mwaka 1958 Baraza la Pili la Waandishi na Wachoraji Weusi lilipitisha Azimio la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano kwa bara zima la Afrika.

Aidha, pendekezo la kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi Afrika liliwasilishwa na Mawaziri wa Afrika wa Utamaduni wakati wa Mkutano wa OAU uliofanyika Port Louis, Mauritius mwaka 1986.

Msukumo ulifanyika pia katika Muendelezo wa Tamasha la Kwanza la Kuhanikiza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya Afrika uliofanyika Zanzibar 1986.

Sambamba na juhudi hizo, viongozi wa nchi za Afrika walikutana katika Mkutano wa Kilele mwezi Julai 2002 jijini Durban, Afrika ya Kusini na kutangaza kwa pamoja kuwa Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za kiutendaji za Umoja wa Nchi Huru za Afrika (Sasa Umoja wa Afrika).

Hatimaye mnamo tarehe 25 Mei 2021, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, alitangaza kuwa lugha ya Kiswahili imepitishwa rasmi kutumika kama lugha ya mawasiliano katika mikutano rasmi ya Umoja wa Afrika.

Kukubalika kwa Kiswahili kama lugha ya Mawasiliano katika Mikutano Rasmi ya Umoja wa Afrika, kunaonesha wazi kuwa kuanzia mwanzoni mwa karne ya 21 lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa sana.

Uamuzi Umoja wa Afrika kuipitisha lugha ya Kiswahili umetokana na kutambua utimilifu wa lugha ya Kiswahili.

Pia, historia ya Kiswahili katika ujenzi wa amani ni kubwa mno, na hivyo kuipa nafasi kupenya katika korido za Umoja wa Mataifa.

Katika muendelezo huo, mwezi Machi mwaka 2021, Tanzania iliomba Kiswahili kitumike katika kuendeshea mikutano ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi za SADC ili kukifanya kuwa lugha rasmi ya kuendeshea mikutano ya SADC.

Hili lilifuatia mapendekezo ya Kamati Maalumu iliyopitisha mapendekezo hayo mwezi Agosti 2019, katika mkutano wa Kilele wa SADC uliofanyika Dar es Salaam.

Kutokana na mafanikio hayo, Kiswahili ni fursa adhimu kwa serikali, wafanyabiashara,wajasiliamali na wananchi wa kawaida katika kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi, kisiasa na kijamii Afrika na duniani kwa ujumla. Kwa nini?

Kwa sababu mwaka 2013 wakati Umoja wa Afrika ukitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963, nchi za Afrika zilikuja na mpango wa maendeleo wa Afrika ujulikanao kama Ajenda 2063 ambayo inalenga kuliunganisha bara la Afrika katika nyanja zote: kijamii, kisiasa, kisayansi, kiuchumi, kibiashara na kiutamaduni.

Kutokana na mpango huo mkakati wa Afrika 2063 na utumikaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano utainufaisha sana Tanzania kuweza kuyafikia malengo yake ya kisera.

Ni wazi kuwa Kingereza ambacho bado kinaonekana kama lugha ya kikoloni hakiwezi kuinufaisha Tanzania kufikia malengo yake ya kisera.

Aidha, si Kifaransa ambacho nchi pekee zinazongumza ni zile za Kaskazini na Magharibi mwa Afrika na Kati kidogo, sambamba na Burundi, DRC na Rwanda.

Vilevile, si Kichina ambacho ndiyo kwanza kinaanza kufundishwa Afrika hakiwezi kabisa kuwa lugha yetu ya mawasiliano.

Kadhalika, si Kireno ambacho kinazungumzwa Angola, Msumbiji, Guinea-Bissau, Cape Verde, São Tomé na Príncipe na kidogo Guinea ya Ikweta. Au Kihispaniola ambacho kinazungumzwa Guinea ya Ikweta pekee.

Kwa kutazama changamoto ya lugha nyingine tunaona kuwa ni wazi kuwa Kiswahili pekee ndicho ambacho kinaweza kutumika kuziunganisha nchi za Afrika.

Hilo litainufaisha sana Tanzania kuongeza ushawishi katika maamuzi ya kisera na ya kimkakati ndani ya Umoja wa Afrika.

Katika kuthibitsha hilo, Adebayo na wenzake katika kitabu chao Marginality and Crisis cha mwaka 2010 waliandika:
Kiswahili kimetambuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kama lugha yenye kuleta umoja katika nyanja za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu, kisayansi na kiteknolojia.

Hivyo ni wazi kama Tanzania itatumia fursa ya Kiswahili vizuri itafikia baadhi ya malengo yake na kuongeza ushawishi katika siasa za Kimataifa na Diplomasia na kuleta ukombozi wa kweli Afrika.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa na kongwe duniani ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uhusiano wa kidiplomasia kabla na baada ya uhuru wa bara la Afrika.

Kihistoria, Kiswahili imekuwa lugha ya mawasiliano kwa jamii ya mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki tangu karne ya kumi na nne.

Ni lugha ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni mia moja ishirini katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. (Adebayo na wenzake, 2010:64). Kwa sasa lugha hii inazungumzwa na watu zaidi ya milioni mia mbili duniani.

Kiswahili ni lugha inayozungumzwa katika mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika ya Kusini. Hivyo ni lugha inayozungumzwa na mataifa mengi Afrika.

Kidiplomasia ukuaji wa ushirikiano kati ya ukanda wa Afrika Mashariki na Mashariki ya Mbali pamoja na Mashariki ya Kati ulitegemea ukuaji wa Kiswahili.

Hivyo, Kiswahili kimetumika kama kiungo kati ya wafanyabiashara wa nje na wa ndani kukuza Diplomasia ya Uchumi.

Kwa upande mwingine lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa bara la Afrika.

Kiswahili ndiyo lugha iliyotumiwa na chama cha TANU kuwaunganisha watu na kufanikisha ukombozi na uhuru wa Tanganyika.

Kiswahili kilikuwa pia lugha ya ukombozi na kilitumika kama nyenzo ya mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964.

Kiswahili ndiyo lugha iliyoziunganisha Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili 1964.

Lugha ya Kiswahili ilitumika kama lugha ya ukombozi wa nchi za Kusini na Kaskazini mwa Afrika.

Mashujaa wa FRELIMO,PAC,ANC,MPLA, POLISARIO na ZANU-PF walipokea mafunzo yao na msaada wa ukombozi kwa mchango wa Kiswahili kama lugha iliyowaunganisha.

Hivyo, katika hatua za awali za utekelezaji wa sera ya kwanza ya mambo ya nje ya Tanzania lugha ya Kiswahili ilikuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wake, hususan kwenye eneo la ukombozi.

Mbali na hayo, Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya Ukombozi wa bara zima la Afrika huku Tanzania ikiwa ndiyo kitovu cha harakati hizo chini ya Kamati ya Ukombozi iliyoongozwa na Hatayi Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

Hili lilielezwa kwa kina na Khatib (2004) akielezea uwezo wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya ukombozi wa waafrika.

Khatib alieleza kwa mawanda mapana namna nasaba ya Abushiri ilivyoweza kutumia Kiswahili kupambana na uvamizi wa waarabu katika karne ya Kumi na Saba.

Kwa umuhimu wa kipekee, Kiswahili kilitumika pia kama lugha ya ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Afrika ya Kusini (wakati wa ubaguzi wa rangi), Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika ya Kati na Kongo.

Kiswahili pia kinatumika kama lugha ya utafiti katika vyuo vikuu mbalimbali vya Afrika, Ulaya, Asia, na Marekani.

Kutokana na nafasi hiyo ya Kiswahili taasisi mbalimbali za kimataifa husaidia tafiti katika elimu ya Kiswahili.

Hizi ni miongoni mwa sababu zilizofanya Sekretarieti ya Umoja wa Afrika (AU) kukichagua Kiswahili kama lugha yake rasmi ya kazi (Adebayo na wenzake, 2010:65).

Tunapozungumzia utaifa na demokrasia leo hii katika Afrika tunapaswa kufahamu kuwa msingi wake ni lugha ya Kiswahili.

Katika kuthibitisha hili Muthwii na Kioko (2004) wameandika:
Lugha ni chombo muhimu katika kuhanikiza utaifa.

Kwa msingi huo Kiswahili kina umuhimu mkubwa katika kuanzishwa kwa demokrasia ya kweli na usawa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Ongezeko la matumizi ya Kiswahili katika nchi mbalimbali za Afrika na duniani kwa ujumla kunatoa ishara ya kukua na kuimarika kwa lugha hii.

Ushawishi wa Kiswahili katika majeshi ya Rwanda, Burundi, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kunaonesha ni jinsi ambavyo Kiswahili kinabeba ujumbe wa amani.

Zipo sababu kadhaa zinazoashiria mafanikio haya ya kukua kwa Kiswahili zikiwemo nchi ya Afrika ya Kusini kuanza kukitumia Kiswahili katika mitaala ya shule zake nchini humo katika ngazi mbalimbali.

Kujiunga kwa nchi za Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kunaifanya lugha ya Kiswahili kuwa na nafasi kubwa ya ushawishi Afrika.

Mbali na hilo, kuwepo kwa idhaa za Kiswahili za Mataifa kama Ufaransa (RFI), Marekani (VoA Kiswahili), Uingereza (BBC Kiswahili), Ujerumani (DW Kiswahili), China (CRI), Japan (Redio Japan Kiswahili) sambamba na redio ya Umoja wa Mataifa (UN) inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili kunazidi kuipa kasi lugha hii.

Mbali na nchi hizo na Umoja wa Mataifa, nchi ya Urusi ina vyuo vikuu vutatu vinavyofundisha Kiswahili.

Hivyo, tukiwa kwenye Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika ambao ni mpango mkakati wa kulibadii bara la Afrika katika miaka hamsini ijayo na kuleta maendeleo endelevu, kuna haja ya kujenga misingi imara ya kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kupeleka ushawishi kwenye utendaji wa Umoja wa Afrika.

Bara la Afrika linaongozwa na Dira isemayo Afrika iliyofungamana, yenye maendeleo na amani inayoendeshwa na wananchi wake na inayowakilisha kani isiyosimama katika nyanja za kimataifa.

Katika muktadha huo, kuna haja ya kuathiri wananchi wengi wa nchi za Afrika watumie Kiswahili kama lugha ya mawasiliano. Lakini je tunaanzia wapi?

Hilo ndilo suala la msingi lakini naamini ipo sehemu ya kuanzia. Tunahitaji kuanza na haya yafuatayo:

Kiswahili kinaweza kutumika kama nyenzo ya ushawishi ambayo kwa lugha ya Kingereza huitwa ‘soft power’ yaani nguvu ya ushawishi isiyo ya shuruti. Ni kwa vipi Kiswahili kinaweza kuwa nguvu ya ushawishi isiyo na shuruti?

Joseph Nye ameifafanua nguvu hii isiyo na shuruti kwa kusema kwa lugha ya Kingereza kama ifuatavyo:

‘Soft power is the ability to set the agenda in world politics through persuasion, enticing and attracting others through the force of one’s beliefs, values and ideas, and not through military or economic coercion’ (Nye, 1990:176).

Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi; Nguvu isiyo na shuruti ni uwezo wa kujenga ajenda/hoja katika siasa za dunia kupitia ushawishi na kuwavutia wengine kupitia nguvu ya imani ya mtu, misingi na mawazo, na si kupitia majeshi au vikwazo kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo Tanzania inaweza kupenyeza ushawishi wake kwa nchi za Afrika zote zikatumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika nchi zao.

Hilo litawezekana endapo tu Tanzania itakuwa na mkakati madhubuti wa kuitumia lugha hii kufikia malengo hayo.

Kama Tanzania iliweza kujenga hoja za kufanya kuwepo na mabadiliko ya ibara ya 25 ya Sheria ya Kimamlaka ya Afrika (African Union Constitutive Act), kulikopelekea kuondolewa kwa maneno ‘working languages’ na kuwekwa maneno ‘official languages’ kama ilivyoelekeza ibara ya 11 sheria ndogo ya mabadiliko kwenye Mkataba wa Kimamlaka wa Afrika yaani Protocol on Amendments to the Constitutive Act of the African Union, basi Tanzania inaweza kujipanga kuifanya lugha ya Kiswahili iwe lugha ya kila taifa la Afrika.

Kwa kuanzia, Tanzania inaweza kuanzia kwa mabalozi waliopo nchini wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Serikali inaweza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha mabalozi wote wa nchi za kigeni wanapatiwa mafunzo ya Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia (CFR) kilicho chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mtu anaweza kuuliza kwa nini Chuo cha Diplomasia?

Kwa sababu Chuo cha Diplomasia si Chuo tu bali ni Kituo chenye hadhi ya kibalozi.

Hadhi hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1986 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohusu Upendeleo na Kinga za Mabalozi.

Sheria hiyo ilitungwa kuridhia Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na ule wa 1963 inayohusu Mahusiano ya Kidiplomasia na Kikonseli mutawalia.

Hivyo Chuo hicho kinakidhi kufundisha lugha ya Kiswahili kwa mabalozi kwa sababu ya kuwa na hadhi ya kibalozi (Kinga).

Pili Chuo cha Diplomasia (CFR) ni sehemu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika inayotambuliwa na Umoja wa Afrika.

Ikumbukwe kuwa, kabla ya Makubaliano ya Nchi za Msumbiji na Tanzania mnamo tarehe 13 Januari 1978, awali Chuo hicho kilitumika kama Taasisi ya Elimu ya Juu ya wapigania Ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Hivyo, kwa hadhi ya kibalozi na historia inayokibeba ni sehemu muhimu na nzuri ya kuwafundisha mabalozi Kiswahili.

Aidha, Tanzania inahitaji kujenga vituo vya kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi mkakati kama Nigeria, Misri, Senegal, DRC na Afrika Kusini, vituo hivi vitasaidia kueneza na kusambaza Kiswahili katika nchi hizo na jirani.

Vilevile, balozi zote za Tanzania zinaweza kuwekewa kiunganishi (link) maalumu kwa wageni kujifunza Kiswahili katika tovuti za Balozi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuwavutia wageni kukijua Kiswahili.

Pia, kuwa na Tamasha kubwa Kiswahili Afrika ambalo litakuwa likifanyika hapa Tanzania kila tarehe 7 Julai ni jambo muhimu.

Kadhalika, kunaweza kukaandaliwa mashindano ya usomaji Kiswahili na uandaaji wa insha kwa wageni.

Hayo yanawezekana kwa sababu tayari Umoja wa Afrika umeazimia kujenga Kituo Kikuu cha Urithi wa Ukombozi Afrika nchini Tanzania.

Hivyo, kupitia kituo hicho Tanzania inaweza kupenyeza ushawishi wake kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya waafrika wote.

Sambamba na hayo, kufuatia uwepo wa ujenzi wa Kituo hicho cha Urithi wa Ukombozi, Tanzania inaweza kujenga kituo cha Utafiti (Research Centre) ambacho licha ya kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya kisera Afrika, kituo hicho kitakuwa kikifanya utafiti wa lugha mbalimbali za Afrika ili kuipa lugha ya Kiswahili misamiati mingi zaidi kutoka katika lugha hizo, na hivyo kuongeza ushawishi zaidi na kuifanya lugha hii ikubalike Afrika nzima.

Ninaamini ili kufikia dira ya Afrika 2063 lugha ya Kiswahili ndiyo itakuwa kiunganishi pekee ambacho ni fahari ya waafrika.

Ni moja ya vielelezo vya kujitawala. Aidha kwa kiasi kikubwa ni lugha ya maendeleo ya mwafrika.

Hivyo basi mikakati madhubuti inahitajika kukifanya Kiswahili kitumike Afrika nzima na Tanzania inufaike kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kwa bahati mbaya sana, katika hali ya kushangaza, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) mwezi Juni 2023 lilipiga marufuku kutumia Kiswahili katika vikao vyake licha ya lugha hiyo kupitishwa kama lugha rasmi ya vikao vya EALA.

Je Tanzania inalichukuliaje hili?

Bahati mbaya nyingine ni kwamba, matangazo ya kukitangaza Kiswahili na mialiko inatoka kwa lugha ya Kingereza na lugha nyingine za kigeni? Tunakuzaje Kiswahili katika hali hii?

Mitaala yetu ya elimu bado inakipigia chapuo Kingereza ingawa tunataka kukifanya Kiswahili kuwa nyenzo. Inawezekanaje?

Ndiyo maana kichwa cha habari kimekuja kwa kuuliza, ‘Kiswahili:Nyenzo iliyokosa uelekeo?’

Abbas Mwalimu
 Abbas Mwalimu 
Back to top button