Habari Tofauti

TUSIKILIZE MAKUNDI YOTE YA WANANCHI HASA WASIO NA CHA KUTULIPA

0:00

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wahitimu wa Vyuo mbalimbali nchini  mara baada ya kuajiriwa au kujiajiri wakasikilize na kuhudumia watu wa makundi yote hasa maskini kwani kila mwananchi ana haki ya kupata huduma bora bila kujali hadhi aliyonayo.

Amesema hayo katika Mahafali ya 26 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT), tarehe 16 Desemba 2023 yaliyofanyika katika Viwanja vya Raila Odinga jijini Mwanza.

“Ndugu Wahitimu na wale ambao tupo makazini, tusikilize watu wa makundi yote hasa wale wasio na kitu cha kutulipa na tuone fahari ya kunyanyua hadhi ya watanzania kwenda kwenye maisha yaliyo bora zaidi kwani ukisaidia maskini unakuwa umesaidia wananchi wengi zaidi.” Amesema Dkt. Biteko

Aidha, Dkt. Biteko ametaka Wahitimu nchini kuchukia rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwaeleza kuwa, waone fahari kuchukia rushwa na waichukie kwa kuonekana kwa macho ili kutoa heshima kwa Vyuo na nchi kwa ujumla.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa kila mtu mwenye juhudi na kuhakikisha kwamba mazingira ya kufanya kazi yanakuwa bora,  pia Serikali itaendelea kuweza mazingira mazuri ya uwekezaji, na kuendelea kuajiri kila itakapopata nafasi za kuajiri wahitimu wenye taaluma mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan  ametuma salam za pongezi kwa Jumuiya ya wana SAUT na wahitimu kwa Mahafali hayo ya 26.

Amesema kuwa, Rais anaamini kwamba, uwepo wa Taasisi hiyo ya SAUT inaongeza mchango mkubwa katika mipango ya Serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi kupitia wahitimu wa kada mbalimbali katika Chuo hicho.

Back to top button