Dkt. Jafo atoa wito wa kulinda na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Tanganyika na rasilimali zake
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito wa kulinda na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Tanganyika na rasilimali zake ili liendelee kuinufaisha jamii na kuleta maendeleo endelevu.
Amesema ni wajibu wetu kuhakikisha changamoto zinazolikabili zikiwemo kupungua kwa kina cha maji, uchafuzi wa mazingira kutoka viwandani na majumbani, upotevu wa bayoanuai na mchanga zinakwisha.
Dkt. Jafo ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Ziwa Tanganyika uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mulungushi jijini Lusaka, Zambia Novemba 17, 2023.
Dkt. Jafo amesema ziwa hilo ni urithi wa shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanywa ndani ya bonde zikiwemo uvuvi, kilimo, ufugaji, makazi ya watu na uchimbaji madini.
“Tutambue kuwa Ziwa Tanganyika ni zaidi ya kapu la chakula kwa jamii zetu na bonde lake ni nyumbani kwa zaidi ya watu milioni 13, ni eneo bora kwa kuunganisha nchi zetu nne zinazolizunguka, hivyo hatuna budi kushirikiana kwa pamoja katika uhifadhi na matumizi sawa ya rasilimali zake,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Jafo amesema kuwa mkutano huo ni muhimu katika kutathmini hatua iliyofikiwa kuelekea matumizi endelevu ya rasilimali na utekelezaji wa miradi chini ya mpango wa kikanda, hii ni fursa ya kutoa mwongozo kuelekea lengo hilo. Mkutano pia umetumika tukio la kutia saini Itifaki ya Maendeleo ya Ufugaji wa Majini katika Ziwa Tanganyika na bonde lake.
Ameshukuru wadau wa maendeleo kwa juhudi zao katika usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika kupitia miradi wanayotekeleza na kusema kuwa Serikali ya Tanzania inalichukulia kwa uzito mkubwa suala la maendeleo endelevu ya Bonde la Ziwa Tanganyika.
Akifunga mkutano huo Dkt. Jafo amempongeza Waziri wa Uchumi wa Kijani na Mazingira wa Serikali ya Zambia Mhe. Mhandisi Dkt. Collins Nzovu kwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza Kuu la Mawaziri.
Katika mkutano huo, washiriki wamepokea na kujadili masuala mbalimbali muhimu yakiwemo taarifa za uchambuzi wa uwezekano wa kuwajumuisha Makatibu Wakuu katika Vyombo vya Sheria vya LTA, Itifaki ya Maendeleo ya Kilimo cha Majini kwa Ziwa Tanganyika na bonde lake;.
Taarifa zingine ni utafiti kuhusu maeneo muhimu ya bioanuwai katika Ziwa Tanganyika na bonde lake, hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, hali ya michango ya kitaifa na mpango wa kazi wa mwaka na bajeti ya LTA ya mwaka 2024.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo wa Burundi ambaye ni mwenyekiti anayemaliza muda wake Mhe. Mhandisi Prosper Dodiko, Waziri wa Uvuvi na mifugo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Adrien Bokele Djema na Mkurugenzi Mtendaji wa LTA Sylvain Tusanga Mukanga.
Ujumbe ulioshiriki katika Mkutano huo uliwashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Deogratius Paul.
Baraza hilo linaundwa na mawaziri kutoka nchi nne ambazo ni Tanzania, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).