DKT.DUGANGE AMSHUKURU RAIS KWA KUTATUA CHANGAMOTO YA ZAHANATI YA MASAULWA
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Dkt Festo Dugange amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza changamoto ya muda mrefu ya Zahanati katika Kijiji cha Masaulwa Kata ya Imalinyi Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.
Mhe.Dkt Dugange ametoa shukrani hizo wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika zahanati hiyo ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wa kijiji hicho.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masaulwa, Dkt. Dugange amesema kijiji hicho kwa muda mrefu kulikuwa hakina Zahanati jambo ambalo lilikuwa linawalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya lakini ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshuhudia changamoto hiyo ikimalizika.
“Tunamshukuru Rais ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake ameleta kiasi ch Sh. Milioni 93.6 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati hii ya kisasa sambamba na watumishi wawili kwa ajili ya kuhudumia afya za wananchi wa Masaulwa.”
” Nimeweka jiwe la msingi kwenye Zahanati yetu na niwape habari njema Mhe. Rais alishatupatia kiasi cha Sh. Milioni 750 kwenye Wilaya yetu ya Wanging’ombe kwa ajili ya vifaa tiba vya maabara, vitanda na vifaa vingine vipo njiani vinakuja. Kwahiyo niwahakikishie zahanati hii itaendelea kuboreshwa kadri muda unavyozidi kwenda,” amesema.
Kuhusu Kituo cha Afya kwenye Kata hiyo ya Imalinyi, Dkt.Dugange amesema serikali imeshapeleka kiasi cha Sh. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kimeshakamilika na kinafanya kazi.
“Kipekee nimshukuru Mhe Rais kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika sekta ya afya katika Wilaya yetu. Ndani ya miaka hii mitatu amekamilisha ujenzi wa vituo vya afya katika kata sita kati ya saba zilizopo kwenye Tarafa hii ya Imalinyi. Haya ni mafanikio makubwa na hatuna budi kumshukuru kwa namna alivyoonesha kujali maisha ya wananchi wa Wanging’ombe,” amesema.