Habari

 RAIS SAMIA: MIRADI YA ELIMU KUPUNGUZA MSONGAMANO WA WANAFUNZI DARASANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema miradi ya Elimu aliyoizindua leo itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zote za msingi na Sekondari na kusogeza huduma ye Elimu karibu na wananchi.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Police Square wilayani humo leo tarehe 15.10.2023.

“Leo nimezindua Shule ya Msingi Imbele iliyoko kwenye Manispaa ya Singida iliyojengwa kupitia mradi wa BOOST na nimeambiwa kuwa shule kama ile zimejengwa nchini kote, pia nimeona kupitia picha shule ya Sekondari iliyojengwa kupitia Mradi wa SEQUIP na zenyewe zimejengwa nchi nzima.”

“Lengo la miradi hii ni kusogeza huduma za Elimu karibu na makazi ya wananchi ili watoto wetu wasitembee umbali mrefu kufuata shule lakini pia kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye madarasa.”

“Pale Imbele niilingia darasani na nikakuta wanafunzi 45 tu tumeshahama kutoka kwenye msongamano wa wanafunzi 120 na sasa tuko kwenye wanafunzi 45 tu ambao ni rahisi kwa mwalimu kufundisha na wakamuelewa na haya ni maendeleo makubwa kwetu na hii ni kote ambako shule hizi zilipojengwa,”amesema Rais Samia.

Amesema dhamira ya serikali ni kujenga shule hizo Tanzania nzima ili wanafunzi wasome katika mazingira bora ya elimu.

Mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano utagharimu sh. Trilioni 1.5 huku Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) utagharimu  Sh. Trilioni 1.1 na zitajenga Shule 1000 za Sekondari kwenye Kata ambazo hazina shule za Sekondari na kwenye shule zenye msongamano wa wanafunzi.

Back to top button