Habari

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS SAMIA JUKWAA LA KIMATAIFA LA CHAKULA, ITALIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Oktoba 14, 2023 amewasili Rome, Italia ambapo atamuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani litakalofanyika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali utaambatana na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO)

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo vijana, wakulima, wazalishaji wadogo, watunga sera, wawekezaji katika kilimo na wanasayansi duniani, wote wakiwa na lengo la kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote na bila kumwacha mtu yoyote nyuma.

Pia, jukwaa hilo litaweka msisitizo kwa nchi husika katika kuchukua hatua za ndani ambazo zinajikita kwenye uvumbuzi, ushirikiano, sayansi, ushirikishwaji wa vijana, wazawa, wanawake na watu walio katika mazingira magumu.

Katika jukwaa hilo la siku nne, Wakuu wa nchi na Serikali kutoka nchi shiriki takribani 31 watapata fursa ya kushiriki katika Mpango wa “Hand-in-Hand Initiative” ambapo watawasilisha mipango ya uwekezaji iliyopewa kipaumbele nchini mwao na kuonesha fursa kwenye maeneo ambayo Mpango huo wa Shirika la Chakula na Kilimo unasaidia Serikali kupunguza umaskini na njaa.

Viongozi Wakuu watakaohudhuria ni Rais wa Italia Mhe. Sergio Mattarella, Rais wa Ireland Mhe. Michael Higgine, Mfalme wa Lesotho, Viongozi wa Ujumbe kutoka Nchi Wanachama, Viongozi Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (FAO, IFAD & WFP).

Back to top button