
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu Dkt. Charles Msonde amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka shuleni watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano 2023 kwa kuwa mioundombinu imekamilika.
Dkt. Msonde ametoa tamko hilo leo Agosti 12, 2023 mara baada ya kukagua miundombinu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha tano katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Amesema wanafunzi 130, 446 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwenye shule 548 kwa mwaka 2023 na kati ya hao wanafunzi wa bweni ni 125, 402 na wanafunzi 5044 ni wanafunzi wa kutwa.
Dkt. Msonde amesema kumekuwepo na ongezeko la wanafunzi, Serikali ilitoa fedha za kuongezea miundombinu ya mabweni ili kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shule ifikapo tarehe 13 Agosti, 2023 kwa ajili ya kuanza masomo.
“Niwatake wazazi na walezi kuhakikisha watoto wetu waliopangiwa kidato cha tano wanaripoti katika Shule walizopangiwa kwa wakati ili waanze masomo kwa wakati tena kwa pamoja ili wasipishane katika masomo.”amesisitiza Dkt. Msonde
Kuhusu wanafunzi walioomba kuhamia shule nyingine, Dkt Msonde amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepokea maombi hayo na kuwataka wanafunzi hao kwenda kuripoti katika shule walizopangiwa kwa sasa.
“Maombi tumeyapokea ila tutayashughulikia wakati wanafunzi wakiwa shule pindi nafasi zinazopatikana kama kuna wanafunzi watakwenda shule binafasi.”
Aidha, Dkt.Msonde amewataka Wakuu wa Shule kuwabadilishia tahasusi wanafunzi walioomba kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI.
“Lakini kwa mwanafunzi anayeomba kubadili tahasusi ambayo haipo kwenye shule aliyochaguliwa anapaswa kuandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu OR-TAMISEMI ili kupelekwa katika Shule husika