Habari Tofauti

KAIRUKI ATETA NA WAWAKILISHI WA SHIRIKA LINALOSAMBAZA UMEME JUA KWENYE VITUO VYA AFYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za mitaa( TAMISEMI), Mh.Angellah Kairuki amefanya mazungumzo na wawakilishi kutoka Shirika la We care la Marekani linalojishughulisha na usambazaji wa umeme jua kwenye vituo vya Afya hapa nchini.

Hadi sasa limesambaza vifaa vya umeme huo katika vituo vya Afya 400 nchini Tanzania huku lengo likiwa ni kuvifikia vituo 5000.

Akizungumza Agosti 6, 2023 jijini Dodoma,  Mh.Kairuki amelishukuru shirika hilo na kuahidi serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya na kupunguza vifo ya mama na Mtoto wakati wa kujifungua.

“Mhe. Rais wetu ni kinara katika kuboresha afya hasa afya ya mama na mtoto kwa kuhakiksha huduma ya uzazi na afya ya mama na mtoto inakuwa salama na yenye utu.Tunaahidi uwzeshaji wowote wa wadau unaleta matokeo chanya,” amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Afya, Lishe na Ustawi wa jamii kutoka TAMISEMI, Dkt.Ntuli Kapologwe amesema kuwa kuna baadhi ya vituo vya afya havijapata huduma ya umeme kutoka gridi ya Taifa hivyo usambazaji wa vifaa hivyo vya umeme jua kutoka The We care Solar utaondoa changamoto hiyo na kuwezesha kila mjamzito anajifungua kwenye mwanga ili kulinda afya ya mama na mtoto.

Kadhalika, Mkurugenzi wa shirika hilo, Amy Donhauser amesema shirika hilo lina uzoefu wa usambazaji wa vifaa hivyo vinavyotengeneza nchini Marekani.

Back to top button