MAWAKALA WA UKUSANYAJI MAPATO KUANZA KUTUMIA MFUMO WA TAUSI
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanya maboresho kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani TAUSI kwa kuziunganisha mashine za POS zote za Mawakala wa Nje katika mfumo huo ili kudhibiti mapato.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka TAMISEMI, Angelista Kihaga alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maofisa Mapato na TEHAMA wa Halmashauri kuhusu mfumo huo uliofanyiwa maboresho kutoka mfumo wa LGRCIS.
Amesema uunganishaji wa Mawakala wote ndani ya mfumo wa TAUSI kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha mbichi na watalazimika kuweka fedha benki (float) kabla ya kukusanya na pale wanapokusanya fedha hizo zitahamishwa kwenye akaunti ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Matumizi ya Mfumo wa TAUSI kwa Mawakala utasaidia kufanya usuluhishi wa kibenki wa miamala kila siku ambapo kama kutakuwepo na miamala ambayo itakuwa na changamoto itashughulikiwa kwa wakati kabla ya kupelekwa katika akaunti ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ” amesisitiza Kihaga
Pia amesema matumizi ya mfumo huo kutasaidia upatikanaji wa taarifa kwa Mawakala kwa wakati na kuwezesha madai ya kulipwa gharama za uwakala kwa wakati.
Aidha,amewataka maafisa hao kuwa waadilifu na waaminifu katika kusimamia mfumo huo na kutoa huduma kwa weledi kwa walipa kodi.