Habari Tofauti

SERIKALI KULIONDOA TATIZO LA UKATILI WA KIJINSIA ZANZIBAR

Ahmed Hassan

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ametoa shukrani kwa niaba ya Serikali kwa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kwa kuunga mkono jitihada za Serikali kwa maeneo waliyolenga hususani uwezeshaji wa Wanawake  na Vijana kiuchumi wanaojishughulisha na Kilimo cha mwani kwa kuwapa mafunzo na vifaa walivyotafuta kwa juhudi zao , ulinzi wa Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukabaliana na tatizo la udumavu linatokana na lishe duni .

 

Aliyasema hayo alipozindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu wa ZMBF na mradi  wa taulo  za kike wa Tumaini katika Maadhimisho ya Mwaka mmoja wa ZMBF yaliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport leo tarehe 20 Machi ,2023.

Aidha, Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutekeleza  programu mbalimbali za zao la mwani Unguja na Pemba.

Vilevile, ameishukuru Taasisi hiyo kwa juhudi za mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto hapa Zanzibar  kwa kulifanya kuwa agenda na sauti ya waathirika kupata uzito.Alieleza Serikali inaunga mkono juhudi hizo katika jambo hilo  kuliondoa nchini.

Naye, Msarifu Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Mama Mariam Mwinyi amesema ZMBF imejikita kuwainua wakina Mama na Vijana kiuchumi, kuwahakikishia Watoto wa kike na wa kiume ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kulinda utu wao pamoja na kuwawezesha Watoto wa kike kufurahia utoto wao wakiwa katika siku za ada za mwezi kwa kuwapatia Taulo za kike kupitia mradi wa Tumaini.

Back to top button