Habari Tofauti

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO MATANO KUKITANGAZA KISWAHILI

Ahmed Hassan

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waandishi wa habari na wadau wote wa Kiswahili waweke mkakati wa pamoja wa kuitangaza lugha hiyo nje ya nchi.

Mbali na kuitangaza lugha hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amehimiza matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu, kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, kuweka mkakati wa kukibidhaisha Kiswahili kitaifa na kimataifa na kuhakikisha kuwa maelezo ya matumizi ya bidhaa yanawekwa kwa Kiswahili.

Ametoa wito huo jana usiku (Jumapili, Machi 19, 2023) wakati akizungumza na wadau mbalimbali alipokuwa akifunga Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil, Kikwajuni, Zanzibar.

Akisisitiza jukumu la kuhakikisha matumizi ya lugha ya Kiswahili yanavuka mipaka ya nchi, Waziri Mkuu alisema: “Nitoe rai kwa waandishi wa habari kuimarisha ushirikiano na wataalamu wa Kiswahili na taasisi za Kiswahili kuhakikisha kwamba mnaweka mikakati thabiti ya kupenyeza Kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali.”

Akielezea umuhimu wa kufanya tafiti za lugha ya Kiswahili, Waziri Mkuu alisema tafiti zina tabia ya kueleza changamoto na kutafuta majibu. “Kwa hiyo tufanye tafiti, BAKIZA na BAKITA tutumie vyuo vikuu kufanya tafiti na kubainisha majibu haya. Tutumie vizuri fursa ya UNESCO ya tarehe 7 Julai, kila mwaka kwa kuendesha makongamano na kubainisha suluhisho,” alisisitiza.

Akielezea mikakati ya kukibidhaisha Kiswahili, Waziri Mkuu alisema iko fursa ya nchi jirani za Malawi, Msumbiji, Sudan na Congo ambako walimu wanaweza kupata ajira za kufundisha lugha hiyo. “Lazima tujitafakari ni kwa nini Kiswahili kinaenda nchi za jirani lakini walimu wengi wa Kiswahili hawatoki Tanzania Bara au Zanzibar wakati Kiswahili kimezaliwa hapa hapa?”

 

Pia aliwataka mawaziri wa Wizara za Viwanda na Biashara kutoka pande zote za Muungano wahakikishe kwamba bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya hapa nchini na zile zinazoingizwa kutoka nje, zinakuwa na maelezo ya Kiswahili ili kuwapa fursa watumiaji wazitumie wakiwa wanafahamu vema maelekezo yaliyomo kwenye bidhaa hizo.

Back to top button