Uncategorized

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI SEKONDARI YA MBEYA GIRLS

0:00

 

*Awaonya vijana wasizime ndoto za watoto wa kike

*Aweka jiwe la msingi jengo la Mama na Mtoto Hospitali ya Wilaya ya Kyela

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Mbeya (Mbeya Girls) na kuweka jiwe la msingi kwenye shule hiyo.

Akizungumza na wakazi wa kata ya Busale iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kyela jana jioni (Jumapili, Mei 12, 2024) Waziri Mkuu alisema ujenzi wa shule hiyo ni utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya awamu ya sita baada ya kubaini kuwa watoto wengi wa kike hawafanyi vizuri kwenye masomo ya sayansi.

“Shule hizi za wasichana zilianza kujengwa ni kwa sababu tumegundua kuwa tuna idadi ndogo sana ya watoto wa kike ambao wanasoma masomo ya sayansi. Kwa hiyo kila mkoa ulipatiwa fedha kwa ajili ya shule hizi,” alisema.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawalinda watoto wote hasa watoto wa kike na akatumia fursa hiyo kuwaonya vijana wasijaribu kukatisha ndoto za watoto hao kwa kuwaharibia masomo yao.

Amewataka vijana wakae mbali na watoto wa kike na kuwaonya kuwa wakizima ndoto zao kwa kuwapa mimba na kuwakatisha masomo, wataishia jela ambako kifungo chake ni miaka 30.

“Ole wenu vijana, ole wenu mharibu au mkatize ndoto ya mtoto wa kike. Yeyote atakayehusika kukatiza ndoto ya mtoto wa kike, kwanza ujiulize una miaka mingapi halafu ujumlishe na miaka 30,” alisema.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Flora Luhala alisema Mei 2023, walipokea sh. bilioni tatu kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo chini ya mradi wa SEQUIP.

Alisema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 80 na hadi kukamilika kwake utakuwa na jengo moja la utawala, madarasa 12, matundu ya vyoo 16, maabara nne, bwalo moja, jengo moja la huduma ya kwanza (Sick-bay), mabweni nane na nyumba mbili za walimu.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea na mpango wa kuboresha huduma za afya, kwa kujenga miundombinu kuanzia ngazi ya Kanda, Mkoa, Wilaya, Halmashauri hadi kata. “Dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika maeneo yao.”

 

Back to top button