Uncategorized

Dkt Selemani Jafo amesema kuwa Wananchi wa Tanzania Zanzibar wanastahili kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana kwa muda mfupi

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo amesema kuwa Wananchi wa Tanzania Zanzibar wanastahili kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana kwa muda mfupi, ikiwemo miradi ya maendeleo.

Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Waziri Dkt. Jafo ameeleza kuwa uwekezaji katika miradi ya maendeleo unaofanyika chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya Awamu ya Nane ni fursa kubwa kwa wananchi kwani inawaletea kipato pamoja na kukuza uchumi.

Amesema Serikali hiyo imeendelea kuifungua Zanzibar kwa kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, ujenzi, uwanja wa ndege na barabara.

Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa kujengwa kwa miundombinu bora hususan hoteli kumeweza kuimarisha sekta ya utalii hivyo kuwavutia watalii kutoka pembe mbalimbali duniani kufika na kutembelea hatua inayosaidia kuingiza kipato.

Amewapongeza viongozi wa Serikali zote mbili yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Mwinyi kwa kudumisha Muungano kupitia utatuzi wa hoja za Muungano hatua inayochagiza amani na mshikamano kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Amesema viongozi hao wakuu wa Serikali hizo mbili pia wameonesha dhamira ya kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na mapinduzi ya viwanda ambavyo vimekuwa ni sehemu ya uwekezaji na hivyo kukuza uchumi.

Dkt. Jafo amefafanua kuwa viongozi wamefungua milango ya uwekezaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi kwa kujenga na kuimarisha miundombinu muhimu, itakayoweza kutoa fursa za kimaendeleo kwa Wananchi.

Pamoja na hayo, Waziri Dkt. Jafo ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuzingatia uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili dunia.

Amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta zinazoingiza mapato hasa utalii, kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuhifadhi mazingira zikiwemo kupanda miti.

Vilevile, Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi kutunza na kusafisha fukwe zilizopo katika maeneo mbalimbali ili ziwe katika mazingira safi na ya kuvutia ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi wa buluu kama ambavyo unachagizwa na Serikali.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid amesema kwa mkoa huo una miradi ya kitalii isiyopungua 255 na kwa kipindi cha miaka mitatu jumla ya miradi 71 ya kitalii imewekezwa na kutoa fursa za ajira zaidi ya 5,850.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Bw. Shariff Ali Shariff amesema mradi huo umesajiliwa kupitia mwekezaji Kampuni ya Muzamil ya Zanzibar kwa mtaji wa Dola za Kimarekani milioni 8 na kutarajiwa kutoa ajira 200.

Itakumbukwa kuwa kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yanakwenda sanjari na uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi ya maendeleo kinatarajiwa kufanyika Januari 12, 2024.

Back to top button