DKT. BITEKO AAGIZA WIZARA YA MAJI KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA MAJI SAFI NA SALAMA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama ili kuendana na thamani halisi ya miundombinu ya maji iliyojengwa na Serikali kwa gharama kubwa ili kuwapa huduma wananchi kwa ufanisi.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo Jijini Dodoma tarehe 22 Machi, 2024 wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Maji Tanzania ambayo yameenda pamoja na Siku ya Maji Duniani.
Ameagiza Wizara na Mamlaka za Maji zijielekeze kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mabwawa ya kuvuna maji ya mvua katika maeneo yasiyo na vyanzo vya maji vya uhakika na kusisitiza kuwa suala hilo lisisubiri rasilimali fedha ya kutosha bali waanze kutekeleza na rasimali zitaendekea kuja wakati utekelezaji umeshaanza.
Vilevile ametoa wito kwa mwananchi mmoja mmoja, Taasisi za Serikali, Binafsi, Madhehebu ya Dini na makundi mengine kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya Mvua kwenye nyumba zao ili kuimarisha upatikanaji wa maji kutokana na mvua zinavyopatikana.
Akizungumzia hifadhi na utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko amewataka Wananchi wajitokeze kutoa maoni katika mkakati wa hifadhi vyanzo vya maji wakati huu Serikali ikiendelea na utayarishaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ili suala la hifadhi za vyanzo vya maji lipewe kipaumbe kinachostahili.
Aidha ameagiza Bodi za Maji na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza jitihada za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na hata wawekezaji wanapokuja nchini lazima wazingatie utunzaji wa mazingira ili yasiathirike