Habari

Dkt. Selemani Jafo amewahimiza wananchi kuhifadhi mazingira ili kuwezesha upatikanaji wa maji hapa nchin

0:00

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewahimiza wananchi kuhifadhi mazingira ili kuwezesha upatikanaji wa maji hapa nchini.

Amesema kuwa uhai wa vyanzo vya maji vilivyopo nchini unategemea uwepo wa mazingira yaliyohifadhiwa vyema na kulindwa.

Mhe. Dkt. Jafo amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Maji Tanzania na Siku ya Maji Duniani jijini Dodoma leo Machi 22, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko.

Waziri Dkt. Jafo amesema kuwa ajenda ya upandaji wa miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa kila mwaka ni ya muhimu kwani miti ikipandwa kwa wingi ndipo vyanzo vya maji vinaongezeka.

Ameeleza kuwa kwa mwaka huu tayari miti zaidi ya milioni 260 imepandwa katika halmashauri hizo hivyo amewashukuru Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kuhamasisha upandaji wa miti katika halmashauri zao.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameipongeza Wizara ya Maji kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Nimshukuru sana Waziri wa Maji (Mhe. Jumaa Aweso) kwani Wizara yake na Ofisi yetu tunashirikiana kwa karibu sana katika utunzaji wa mazingira ya mabonde na hata kule Mbeya tulipokutana tuliweka mikakati kwa taasisi zilizo chini yetu namna gani zinaweza kushirikiana katika ajenda ya kutunza mazingira,“ ameeleza.

Mhe. Dkt. Jafo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kusimamia vyema mazingira kwani yakiwa salama ndio uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya uhai wa viumbe.

Amezungumzia kuhusu maadhimisho hayo ambapo amefafanua kuwa Siku ya Maji Duniani imetokana na Mkutano wa Mazingira na Maendeleo kupitia Azimio namba 47/193 lililowezesha kutamka kuwa tarehe 22 ya mwezi Machi kila mwaka kuwa ni Siku ya Maji Duniani.

Back to top button