Habari

KAMATI YA TAMISEMI YATOA USHAURI NA KUIELEKEZA MANISPAA YA TABORA

Na. Asila Twaha, Tabora

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa ushauri na kuwataka watendaji waliopewa dhamana  kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya ujenzi wa miradi katika maeneo yao kwa kufika site na sio kukaa ofisinj.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Justine Nyamoga amesema, kama  viongozi watafuatilia miradi ni rahisi kujua changamoto, kasoro za miradi inayotekelezwa  mapema  na kuzifanyia kazi mapema  kabla ya mradi huo haujakamilika chini ya kiwango na kuwa na hasara kubwa baadae.

Amesema fedha nyingi Serikali inatoa  kujenga miundombinu ya elimu  kama miradi hiyo haitasimamiwa vizuri itakua ni hasara kwa Taifa na maana yake  viongozi waliopewa dhamana watakua wameshindwa kumsaidia Mhe.Rais ambaye nia yake nikusaidia wananchi.

Mhe. Nyamoga ameshauri viongozi wa Manispaa ya Tabora kurekebisha kasoro zilizonekana katika shule ya msingi ya Miyemba wakati wa ziara ya Kamato hiyo.

Pia wametoa wito kwa viongozi wote wa  Halmashauri kufuata maelekezo na miongozo ya michoro ya ujenzi wa miradi hiyo ya shule wanayopewa bila ya kusahau kujenga vyumba vya kujihifadhia kwa wanafunzi wa kike.

Kwa upande wa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe.Deogratius Ndejembi ameishukuru Kamati na kusema yote waliyoyaelekeza yatashughulikiwa kwa kufanyiwa kazi mapema.

Aidha,  ameihakikishia Kamati  kuwa hakuna Halmashauri  itakayoenda kinyume na Sheria,Taratibu Kanuni na miongozo inayotolewa na  Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Awali akisoma taarifa ya mradi Mwl. Said Malungula amesema shule ya Msingi Miyemba kwa mwaka wa fedha 2022/23 kupitia mradi wa Kuboresha elimu ya Awali na Msingi(BOOST)  ilipokea  Tshs.milioni 561 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya nadarasa 16, jengo la Utawala 1, matundu  24 ya vyoo.

Back to top button