Habari

BIL.23/- ZIMEELEKEZWA KWENYE MIRADI YA MAENDELEO WANGING’OMBE

ZAIDI ya Sh.Bilioni 23 zimepelekwa katika Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya, elimu na barabara katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange katika ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt.Philip Mpango mkoani humo.

“Mhe. Makamu wa Rais ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Wanging’ombe imepata Sh.Bilioni 23 ambapo kwa mara ya kwanza imepata jengo la wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya Wilaya ambalo limegharimu Sh. Milioni 300 pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Milioni 500.”

” Upatikanaji wa jengo hilo la wagonjwa wa dharura limekuwa msaada kwa wananchi wa Wanging’ombe ambao ilikuwa inawalazimu kusafiri kwenda umbali mrefu kwenye Hospitali za Rufaa ya Mkoa na Kanda kwa ajili ya kupata huduma,” amesema.

Ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili vituo vya afya vitano vyenye thamani ya Sh Bilioni 2.5 vimejengwa katika Wilaya hiyo sambamba na Zahanati 15 ambapo kila moja imegharimu Sh.Milioni 50.

” Katika sekta ya elimu Wilaya ya Wanging’ombe imenufaika na ujio wa ujenzi wa shule kubwa ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa ambayo inajengwa kwenye wilaya hii ambayo kiasi cha Sh. Bilioni 4.1 zimetolewa, sambamba na hiyo tumepatiwa shule tatu za Sekondari kwenye Kata ambazo hazikuwa na shule hii imepelekea kuondoa changamoto ya watoto wetu kutembea umbali mrefu, haya ni mafanikio makubwa sana,” amesema.

Kwa upande wa barabara, Dkt. Dugange amesema ndani ya kipindi hicho serikali imetoa kiasi cha Sh.Bilioni 15 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara za mjini na vijijini jambo ambalo litarahisisha wananchi wa Wanging’ombe kusafirisha mazao yao kwa haraka na kukuza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kwa Taifa kwa ujumla.

Back to top button