Habari Tofauti

KAMATI YA TAMISEMI YARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA UTEKELEZAJI WA  MRADI WA TACTIC – MOROGORO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Uimarishaji Miji (Urban Local Government Strenghtening Programme) uliotekelezwa kwenye Manispaa ya Morogoro na maandalizi ya Utekelezaji wa TACTIC na kutoa mapendekezo ya kuboresha katika miradi mingine itakayotekelezwa mkoani humo.

Mapema Oktoba 11 Kamati hiyo imefanya ziara na kukagua baadhi ya miradi ya ULGSP ikiwemo Soko kuu la Chifu Kingalu, Kituo cha dala dala cha Mafiga pamoja na kukagua barabara za nane nane na Tubuyu.

Akitoa mrejesho wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Denis Londo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mkoani Morogoro amesema kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi waliyoitembelea, na kuutaka uongozi wa Mkoa na Halmashauri kuendelea kusimamia kwa makini mradi wa TACTIC unaoanza kutekelezwa sasa.

Aidha, Kamati imemuagiza Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima kuchunguza kwa kina suala la uuzwaji wa eneo karibu na soko kuu la Chifu Kingalu ambalo lilitakiwa kujengwa kituo cha dala dala ambacho kimejengwa Mafiga ili kubaini gharama na mhusika aliyenunua eneo hilo.

Pia, Kamati  imeshauri Mkoa kuangalia namna ya kuwapunguzia waendesha piki piki (Bodaboda) ushuru wa kuingia kituo cha dala dala cha Mafiga ambao wanatozwa kiasi cha shilingi mia tano kila anapoingia.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima ameishukuru Kamati hiyo kwa ziara yake  Mkoani humo na kuahidi kuwa Mkoa itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na Wajumbe wa Kamati  ili kuboresha utekelezaji wa mradi wa TACTIC.

Back to top button