Habari Tofauti

 Serikali isema lengo kubwa katika uhifadhi wa mazingira nchini ni kuhakikisha taifa linakuwa la kijani

 Serikali imesema lengo kubwa katika uhifadhi wa mazingira nchini ni kuhakikisha taifa linakuwa la kijani, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kutunza mazingira yanayomzunguka ili kufanikisha zoezi hilo.

Hayo yamesema leo Oktoba 12, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis alipozungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa inayofanyika Babati, mkoani Manyara kuanzia Oktoba 8 hadi Oktoba 14 ambapo inakwenda sambamba na uzimwaji wa Mwenge wa Uhuru 2023.

Amesema wananchi wanatakiwa kutambua umefika wakati wa kutumia nishati mbadala kwa kutumia gesi, umeme, ganiki, jua na upepo ikiwa ni madhumuni ya kunusuru mazingira ili kuwa na Tanzania ya Kijani.

“Hatutaweza kuwa na Tanzania ya kijani kama tutakuwa tunakata miti, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kutunza mazingira kwa faida ya taifa letu huku elimu ya biashara ya kaboni na matumizi ya nishati mbadala ikiendelea kutolewa zaidi na kuonyesha faida zake.”

“Tuonyeshe huduma za kijamii zilizojengwa kutokana na fedhazilizopatikana kwa kufanya biashara ya kaboni, kuna baadhi ya mikoa kama vile Katavi, Tabora na Geita wamejenga shule, miradi mikubwa ya maji na zahanati, hivyo tuwaambie wananchi hii biashara inatokana na nini na inafanywaje.”

Pia alisisitiza juu ya elimu ya Muungano ambapo amesema Muungano na Mapinduzi ni vitu ambavyo vinakwenda sambamba, hivyo tunapotoa elimu ya Muungano lazima tuelezee na mambo ya Mapinduzi, Zanzibar ilipata uhuru kupitia mapinduzi wakati bara ilipata uhuru kwa maridhiano.

“Tuwafundishe watu kuhusu mapinduzi wajue kuna mapinduzi yalitokea Zanzibar na fursa ambazo zinapatikana kupitia hayo mapinduzi ili kila mmoja aweze kupata ufahamu wa haya mambo,” amesema Mhe, Khamis.

Hoja za Muungano zimeendelea kupungua tangu kuundwa kwa kamati ya pamoja ya SJMT na SMZ za kushughulikia changamoto za Muungano.

Back to top button