Habari

Dkt.Mahera aagiza usimamizi wa karibu ujenzi kituo cha Afya Levolosi

0:00

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Wilson Mahera Charles amemwelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kusimamia kwa karibu ujenzi wa  Kituo cha Afya cha Levolosi unaogharimu Sh.Bilioni1.2 ili ukamilike kwa wakati.

Dkt. Mahela ametoa maelekezo hayo jijini Arusha baada ya kutembelea kituo hicho ambacho kwa mara ya kwanza kilitengewa kiasi cha sh.milioni 500 Septemba 2022 na kusimama kufuatia mabadiliko ya ujenzi kutoka kwenye ‘Force account’ kwenda kwa mkandarasi kutokana na aina ya majengo ya ghorofa yanayojengwa.

Amesema wananchi wanahitaji kuona jengo hilo linakamilika na kuanza kutoa huduma.

Aidha, Dkt. Mahera amepongeza hatua ya ujenzi ilivyoanza na amefurahishwa na ubunifu wa Mkurugenzi wa Jiji kwa kuazima mifuko ya saruji 2000 ili kumpatia mkandarasi wa jengo hilo.

“Timu ya usimamizi ya Mkoa pamoja na mkurugenzi simamieni ipasavyo jengo liweze kukamilika kwa haraka ili azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma kwa wananchi kwa viwango vya nchi iweze kuongezeka,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa  Halmashauri ya Jiji la Arusha, Mhandisi Juma Hamsini amesema jengo hilo ni la  ghorofa tatu na jengo la chini linatarajiwa kuanza kutumika Desemba 2023.

“Kulingana na wingi wa wananchi wanaohitaji huduma hasa huduma ya akina mama peke yao kujifungua kwa upasuaji ni zaidi ya 320 kwa mwezi ndio maana tukasema tupeleke nguvu ya ziada na tuongeze na kasi ya ujenzi na sisi kama Halmashauri tumemuazima mifuko 2000 ya saruji ya kuanzia ili mkandarasi asikwame,” amesema.

Back to top button