Dkt. Jafo akutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Oktoba 9, 2023 katika Ofisi ndogo za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo amepokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa mashirika hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa GEF uliofanyika katika Mji wa Vancouver nchini Canada ambapo ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani.
Amesema Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Akitolea mfano Dkt. Muyungi amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi katika maeneo ya barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa udongo baharini.