Habari Tofauti

Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka Maafisa Ardhi nchini kutoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya ardhi

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka Maafisa Ardhi nchini kutoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya ardhi ili kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.

Ametoa agizo hilo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wakati wa uzinduzi wa Kampeni Maalumu ya ‘Tutunzane Mvomero‘ yenye lengo la kuepusha migogoro ya makundi hayo mawili.

Mhe. Khamis amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kuepuka kukata miti ovyo pamoja na ufugaji usio wa kisasa unaosababisha uharibifu wa mazingira.

Amesema kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji inasababisha uharibifu mkubwa ukiwemo wa mazao, mifugo kuuliwa na kuacha majeraha na vifo kwa binadamu.

“Tupunguze migogoro ya wakulima na wafugaji hebu twendeni tukawafundishe watu wetu namna bora ya kusimamia matumizi ya ardhi ninaamini kila wilaya ina maafisa ardhi, na hili ni agizo la Serikali,“ amesema.

Aidha, kutokana na changamoto ya ukataji miti ovyo, Naibu Waziri Khamis na kwa vile sekta za mazingira, nishati na ardhi ni mtambuka ametoa wito kwa maafisa hao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia.

“Miti inakatwa sana mimi nimetokea Dar es Salaam nimepita barabarani hasa maeneo ya Morogoro na Pwani unapishana na pikipiki zimepakia mkaa, kama mtakumbuka Rais wetu alifungua mjadala wa nishati safi ya kupikia, maana yake anataka tufanye transormation ya nishati tutoke kwemye kuni na mkaa twende kwenye mishati nyingine ya gesi au umeme,“ amesisitiza.

Pia, Naibu Waziri Khamis amesisitiza wananchi waendelee kupanda miti ikiwa ni maelekezo ya Serikali na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kuwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka ili kuifanya nchi kuwa ya kijani.

Back to top button