Habari Tofauti

KAMATI YA LAAC YAPONGEZA USIMAMIZI NA MATUMIZI MAZURI YA FEDHA UJENZI WA SHULE MPYA  MOLETI- KONGWA

Asila Twaha, Kongwa

0:00

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) imeupongeza uongozi wa kijiji cha Moleti Kata ya Chiwe, Halmashauri ya Kongwa kwa usimamizi na matumizi  ya fedha iliyopelekwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi kupitia Mradi wa BOOST.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mhe.Stanslaus Mabula ametoa pongezi hizo Agosti 19, 2023  kwa niaba ya wajumbe wa Kamati wakati wa ziara kijijini Moleti kukagua utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya iliyojengwa kupitia Mradi wa BOOST uliogharimu shilingi milioni 318.

Mhe. Mabula amesema moja ya jukumu la Kamati yake ni kusimamia matumizi ya fedha zinazopelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zinatumika vizuri  na matumizi yake yalingane na thamani ya fedha iliyotolewa kwenye mradi husika.

Akiongea kwa niaba ya Kamati, Mhe.Mabula ameridhishwa na usimamizi  na matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya Moleti yenye vyumba 7 vya madarasa, vyoo matundu 8 vya wanafunzi, vyoo matundu 2 vya walimu, vyumba 2 vya madarasa ya mfano ya wanafunzi wa elimu ya awali, kichomea taka,  jengo la utawala na utengenezaji wa madawati kwa ajili ya shule ya msingi pamoja na meza na viti kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya awali.

Ametoa wito kwa uongozi wa Kijiji kuendelea kushirikiana  katika masuala  ya maendeleo kijiji chao kama walivyoshirikiana kwa  kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na kuwataka kuwasimamia wanafunzi wasome ili wafikie malengo yao bila kuwakatisha masomo.

“Serikali inaleta miradi hii kwa ajili ya wananchi  tuitunze, tuilinde lakini muhimu zaidi nasisitiza tuhimize watoto wetu wapate elimu, miundombinu hii ya shule imekamilika ni jukumu letu wazazi na  walimu amesema Mhe. Mabula.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi  wa shule hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi  Moleti Rose Justine amesema, shule hiyo imepunguza uhaba wa miundombinu  na  imesaidia  kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kutokana na mazingira yake kuwa mazuri.

Vilevile  ameiomba Kamati ya LAAC kiasi cha fedha cha shilingi milioni 10 kilichobaki zitumike kwa ajili ya  uchimbaji wa kisima cha maji  ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji jambo ambalo Kamati imeridhia.

Back to top button