TAMISEMI MSHINDI WA PILI NANENANE KANDA YA KATI

Ofis ya Rais TAMISEMI imeibuka mshindi wa pili katika kundi la Wizara za Serikali kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Nzuguni Jijini Dodoma ambayo yamefikia tamati leo.
Maonesho hayo ya Nanenane yamehitimishwa hivi leo tarehe 8 Agosti, 2023 ambapo Ofisi ya Rais imefanikiwa kupata cheti kilichopokelewa na Mratibu wa Maonesho wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Kanda ya Kati Bi. Hoffu Mwakaja.
Maonesho hato yamehitimishwa na Mhe. Patrobas Katambi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu na kusema Serikali inatambua mchango wa wakulima na ndio maana inaweka mipango thabiti ya kilimo kuwa endelevu na kukifanya kuongeza wigo wa ajira ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo inayokaribia shilingi Trilioni moja kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024.
Katambi amesema Serikali inaendelea kutatua changamoto za kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mifugo, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, huduma za ugani, kujenga miundominu ya mifugo, kufanya utafiti wa kilimo na mifugo pamoja na kuendesha kilimo cha kiteknolojia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule akitoa salamu za utangulizi amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maonesho ya Kanda ya Kati kuwa endelevu badala ya kusubiri kipindi cha mwezi Agosti ya kila mwaka kwani itainua pato la mkulima na mfugaji.
Kwa upande wake Peter Serukamba Mkuu wa Mkoa wa Singida akitoa neno la awali amesema wakulima wa Kanda ya Kati walipata fursa ya kuhudhuria makongamano ya mazao ya mtama na alizeti lakini pia wafugaji walipata fursa ya shindano la nyama choma na paredi ya mifugo ambayo itasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kilimo na kuwaongezea uzoefu.
Mgeni rasmi Mhe. Patrobas Katambi Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho likiwemo banda la Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kujionea mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na mifugo pamoja na vikundi vilivyojipatia fedha za mikopo ya asilimia 10 vinavyofanya shughuli za usindikaji wa mazao ya kilimo