DK.MOLLEL ATAKA USHIRIKISHWAJI VIONGOZI WA CHINI MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA

Naibu waziri wa Afya, Mhe.Godwin Mollel amehimiza ushirikishwaji wa viongozi na jamii ngazi ya chini katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.
Akizundua Agosti 7, 2023 mpango wa ugawaji vyandarua vyenye dawa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, amesema “Hawa viongozi wa wilaya ,kata na vijiji ndo wanaoishi na jamii huku chini hivyo inatakiwa kushirikishwa kikamilifu katika mapambano haya wao ndio watajua kama vyandarua vinatumika kweli au vinatumika kwa kazi nyingine kama kufugia kuku na kuweka uzio kwenye bustani za mboga mboga.”
Amesema mradi huo unalenga kugawa vyandarua vyenye dawa 1,663,262 katika Mkoa wa Kagera vitakavyonufaisha wananchi 3,030,343.
Naye, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapologwe amesema ofisi hiyo imewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini kutenga fedha za kununua viatilifu kwenye kiwanda kilichopo Kibaha mkoani Pwani ili kutokomeza masalia ya mbu.
Mradi huo wa usambazaji vyandarua hivyo utagharimu sh.bilioni 4.8 kwenye Mikoa ya Kagera na Tabora na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Mpango wa Kudhibiti Malaria wa Rais wa Marekani, Naomi Serbantez, amesema kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kufikia lengo la kumaliza ugonjwa huo kwa kutoa
rasilimali fedha , elimu kwa wananchi na ununuzi wa vifaa tiba na teknolojia ya kutokomeza mazalia ya mbu.