Timu ya wataalamu wa Wizara ya Maji ipo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI)
Mpango huo unaojulikana pia kama Blueprint, unalenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kupunguza au kuondoa changamoto mbalimbali zinazodhoofisha maendeleo ya uwekezaji na biashara.
MKUMBI unalenga kukabiliana na Changamoto hizo kwa kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni za kisekta, matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kutoa huduma, kuunganisha majukumu ya mamlaka za udhibiti yatakayobainika kuwa na muingiliano; pamoja na uanzishaji wa vituo vya utoaji wa huduma mahali pamoja.
Wizara ya Maji kama sekta muhimu ya kiuchumi na kijamii ambayo inahusika moja kwa moja na maisha ya wananchi inatambua umuhimu wa mpango huo na imejipanga kuhakikisha uwekezaji unaotegemea huduma ya maji ya uhakika unarahisishwa na hatimaye kusukuma maendeleo ya taifa.
Kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi kimewakutanisha wataalamu wa Wizara, Bodi ya Maji Bonde la Pangani na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi ambao wamejadiliana masuala mbalimbali ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia utoaji wa vibali vya matumizi ya maji, hali ya huduma ya maji kwa ujumla na kuweka mikakati ya kuboresha mazingira ya biashara katika Sekta ya Maji.
Wizara imejipanga kujenga uelewa kwa wadau wa Sekta ya Maji kuhusu mpango wa MKUMBI kwa lengo la kuvutia uwekezaji endelevu unaozingatia maendeleo ya Sekta ya Maji.