Uchumi

WANANCHI JIFUNZENI KUPITIA MAONESHO YA NANENANE – SENYAMULE

Na Fred Kibano – Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Sitaki Senyamule amefungua maonesho ya wakulima Nanenane Kanda ya Kati leo tarehe 02 Agosti, 2023 Jijini Dodoma na kuwaasa wananchi kuhudhuria kwa wingi ili kujifunza mbinu za kisasa za kiteknolojia kwenye kilimo na ufugaji.

Senyamule pia amewataka wananchi wa Singida na Dodoma (Kanda ya Kati) kuungana katika vikundi ili iwe rahisi kwa Serikali kuwawezesha kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo na mifugo kwa lengo la kuongeza kipato lakini pia kufikia nia ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa Tanzania ya wazalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo pamoja na kuuza mazao yaliyosindikwa badala ya mazao ghafi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi Bilioni 34.17ujenzi wa mradi wa umwagiliaji uliopo katika halmashauri ya Wilaya ya Mkalama lakini pia amesema mkoa wa Singida umeendelea kuzalisha ziada ya chakula kwa muda wa miaka mitatu mfululizo na kwamba maonesho hayo ya Kanda ya Kati yatakuwa chachu kwa wakulima na wafugaji katika kujiongezea kipato.

Awali Mheshimiwa Senyamule  aliambatana na mgeni wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba na kupata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya Ofisi za Serikali, Taasisi za Serikali na Binafsi na watu binafsi wanaotekeleza kazi za utoaji wa huduma za kilimo, uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na teknolojia mbalimbali hususani kilimo.

Maonesho hayo yamefunguliwa leo na yatafungwa tarehe 10 Agosti, 2023 ambayo yanafanyika katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.

Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu ni “Vijana na wanawake ni Msingi imara wa Mifumo Endelevu ya hakula”

Back to top button