Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji amekagua mradi wa maji wa Tarime
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja, ame kagua mradi wa maji wa Tarime – Rorya wenye lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa Wilaya ya Rorya, Mji wa Tarime, Sirari pamoja na Vijiji jirani.
Baada ua kukagua mradi huo Mhandisi Luhemeja ametoa maagizo kwa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) kukamilisha mradi huo kwa wakati na hakutakua na muda wa ziada wa kumaliza kazi hiyo.
“Wananchi wanataka maji, hivyo namuagiza Mkandarasi kumaliza mradi huu ndani ya muda, ifikapo mwezi Aprili 2025, Mkandarasi utakabidhi kazi hii, hakutakuwa na muda wowote wa ziada kutekeleza mradi huu.” Mhandisi Luhemeja amesema.
Kwa upande wake mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Maji Mhandisi Joel Rugemalila ameeleza kuwa kazi inaenda vizuri na watahakikisha wanamsimamia Mkandarasi ili akamilishe mradi kwa wakati.
“Mkataba huu ni wa miezi 30, na utakamilika kwa wakati, Wilaya ya Tarime, Rorya na Mji wa Sirari unaenda kuondokana na changamoto ya upatikanaji Majisafi.” Mhandisi Rugemalila amefafanua
Mradi wa maji Tarime-Rorya unahusisha ujenzi wa chanzo chenye uwezo wa kuzalisha maji Lita milioni 29 kwa siku, ujenzi wa Bomba kuu kwa umbali wa Km 90, ujenzi wa matenki matatu (3) yenye ujazo wa lita milioni 6 Rorya, milioni 1 Sirari, na Lita milioni 3 Tarime, ulazaji wa mtandao wa mabonba ya maji kwa umbali wa Km 20 pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kusukuma maji.
Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha zaidi ya wakazi 933,816 katika Vijiji 32 vya Wilaya ya Rorya pamoja na mitaa 81 ya mji wa Tarime.
Aidha mradi huu utaongeza huduma ya upatikanaji majisafi na salama wilayani Rorya kutoka 53.4 inayopatikana sasa hadi kufikia asilimia 90. Kwa upande wa halmashauri ya mji wa Tarime, huduma itapanda kutoka asilimia 63.4 hadi zaidi ya 95.