Habari Tofauti

Zaidi ya nusu ya wakazi Mbogwe wafikishiwa huduma ya majisafi

0:00

Zaidi ya wananchi 142,611, asilimia 55 ya wakazi wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wameondokana na adha ya ukosefu huduma ya majisafi na salama katika maeneo yao baada ya Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji katika makazi yao.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbogwe Mhandisi Rodrick Mbepera amesema kwa sasa kuna miradi zaidi ya kumi iliyokamilika na kutoa huduma.

Mhandisi Mbepera amesema RUWASA inahudumia wananchi kupitia miradi ya maji ya visima virefu, vifupi pamoja na matenki ya kuvuna maji ya mvua na inatarajia kuchimba visima 30 kwa ajili ya kuongeza vyanzo vya maji safi katika wilaya hiyo.

Amesema miongoni mwa miradi ya maji iliyokamilika ni pamoja na mradi wa maji Iponya,Mbope, Nyakafuru, Kagera, Kanegere, Lulembela na mingine ambayo tayari inatoa huduma kwa wananchi.

Mhandisi Mbepera amesema kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Mbogwe umefikia asilimia 55 huku utekelezaji wa miradi mipya ukikamilika utasaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka salimia 55 hadi asilimia 75.

Amesema katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 kuna upanuzi wa mradi wa maji Kanegere, Kagera na Lulembela pamoja ujenzi wa miradi mipya.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita Mhandisi Jabiri Kayilla amesema RUWASA Mkoa wa Geita inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika wilaya hiyo kwa lengo la kutimiza azma ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Amesema miradi ya maji iliyotekelezwa kupitia fedha za UVIKO 19 Wilayani Mbogwe imekamilika kwa asilimia mia na tayari wananchi wa Mbogwe wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mhandisi Kayilla amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kutosha katika utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Geita.

Back to top button