Habari Tofauti

Wafanyakazi wapya wa (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura

Ahmed Hassan

Wafanyakazi wapya Idara ya Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkuu wa timu ya kuratibu jinsi ya kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi na wadharura kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Faraji Lydenge alisema mafunzo hayo yatawasaidia wauguzi hao kuupampu moyo wa mgonjwa uliosimama ili kusaidia damu kwenda kwenye moyo na sehemu nyingine za mwili.
Dkt. Faraji ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha huduma ya dawa za Usingizi kwa wagonjwa wa moyo alisema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi JKCI ili kuifanya taasisi hiyo kuwa kituo cha ubora katika kuhudumia wagonjwa hivyo wakaona kuna umuhimu pia wa kutoa mafunzo hayo mapema kwa waajiriwa hao ambao wameripoti kazini wiki tatu zilizopita.
“Moyo ukishindwa kufanya kazi na kusimama huduma ya dharura isipofanyika ndani ya dakika tano za mwanzo ubongo wa mgonjwa unakosa damu ya kutosha na hewa ya oksijeni ya kutosha hivyo kuleta athari kwa mgonjwa kwani ubongo wake unaweza ukafa, ama mgonjwa akapoteza maisha yake”, alisema Dkt. Faraji.
kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo Afisa Muuguzi Samweli Mpiga alisema waajiriwa wapya katika Taasisi hiyo wameongezewa ufahamu wa kuona viashiria vya mtu ambaye anakwenda kupoteza fahamu, mapigo ya moyo kusimama na upumuaji kusimama.
“Tumewafundisha waajiriwa hawa ambao wako katika Idara ya Uuguzi ili kama watakutana na wagonjwa ambao mioyo yao inaenda kusimama watawasaidia na kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanatutegemea”, alisema Samweli.
Samweli ambaye pia ni Muuguzi katika chumba cha wagonjwa wa dharura na mahututi alisema kupoteza fahamu, mapigo ya moyo kusimama au upumuaji kusimama humtokea mtu yoyote na wakati wowote sio kwa wagonjwa tu hivyo ni muhimu mafunzo hayo watu wote wakayafahamu ili wanapokutana na mtu anayehitaji kupatiwa huduma ya dharura waweze kusaidia na kuokoa maisha yake.
“lengo letu kuu la kufaya mafunzo haya ni kuhakikisha kuwa moyo hausimami maana moyo ndio unaosambaza damu kwenye moyo wenyewe na kwenye ubongo ambavyo hivyo ndivyo viungo vikuu viwili ndani ya mwili havitakiwi kukosa damu”, alisema Samweli.
Naye Muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) Irene Mallya ambaye amepatiwa mafunzo hayo alisema sehemu anayofanya kazi inahitaji kujua jinsi ya kutoa huduma ya kuokoa maisha ya mgonjwa hivyo mafunzo hayo yatamsaidia kufanya majukumu yake vizuri.
“Endapo mgonjwa akipata tatizo la moyo kusimama nitaenda kutumia mafunzo haya kuokoa maisha yake, ninaomba tuendelee kupewa mafunzo mbalimbali ambayo yatatusaidia katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaohitaji huduma zetu”,
“Wauguzi wenzangu tunapopata nafasi ya kujifunza tutumie nafasi hiyo vizuri kwani vitu huwa vinabadilika, tuwe wepesi kutafuta mbinu mpya kuboresha huduma zetu na kuokoa maisha”, alisema Irene.
Back to top button