MCHENGERWA AIBANA KAMPUNI YA NYANZA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Kampuni ya Nyanza Roads Works Ltd isipewe kazi nyingine zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa sababu ya kuchelewa kuanza utekelezaji wa kazi ya ujenzi wa daraja aliyopewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo kwenye hafla ya utiaji saini Mkataba wa uboreshaji wa Miji ya Tanzania (TACTIC) iliyofanyika leo Septemba 23, 2023 jijini Dar es salaam.
Amesema kampuni hiyo imepewa kazi ya ujenzi wa daraja na barabara kwenye Halmashauri hiyo na fedha wameshalipwa lakini mpaka sasa kazi hiyo hawajaanza hivyo baada ya kazi ya leo ya TACTIC wasipewe kazi nyingine mpaka wamalize kazi hizo.
“Kwa hali hii hapa wasipewe kazi nyingine chini ya Wizara hii mpaka hapo watakapokamilisha kazi hii wanayopewa leo na ile ya kule Rufiji, nalielekeza hapa kwa Kampuni hii na itakuwa hivyo kwa mwingine yeyote ambaye hatatekeleza vizuri kazi aliyopewa; Kila mtu afanye kazi kwa weledi na uadilifu kama huwezi kazi usichukue,” amesisitiza Mhe.Mchengerwa.
Mradi huu wa TACTIC unatekelezwa katika Halmashauri 46 nchini na unasimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na utagharimu Dola za Marekani milioni 410.