WANAWAKE WATAKIWA: KUMUENZI BIBI TITI KWA KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI
Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amewataka wanawake nchini kuuenzi mchango wa Biti Titi Mohamed kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.
Dkt. Msonde amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Nyayo za Bibi Titi na Mwalimu Mwanamke kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, lililoandaliwa na Kitengo cha Walimu Wanawake Wilayani Rufiji kwa kushirikiana na UWT mkoa wa Pwani.
Dkt. Msonde amesema, Bibi Titi ameacha funzo la ujasili na ungozi bora kwa wanawake katika taifa, wasisite kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.
Ameongeza kuwa, mchango wa Bibi Titi umeacha alama kubwa kwa taifa na akina mama kwani ametoa somo la ujasiri wa kupambania taifa, kusimama katika uzalendo, uadilifu na uongozi wenye tija.
“Mwakani tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivyo wanawake mjitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kwasababu somo tunalolipata toka kwa Bibi Titi ni ujasiri wa kujitokeza na kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi ili kutoa mchango katika taifa,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Akizungumzia ushirikiano wa CWT Rufiji na UWT Mkoa wa Pwani, Dkt. Msonde amesema amefurahishwa na namna walivyounganisha nguvu na kuwaomba washirikiane katika kutatua changamoto ya utoro wa watoto shuleni wilayani Rufiji ili watoto wote waende shule na wapate ujuzi.
Sanjari na hilo, Dkt. Msonde amesema amelipokea ombi la Kitengo cha Walimu Wanawake Wilayani Rufiji la kutaka mke wa Mhe. Mchengerwa kuwa mlezi wa kitengo chao na kuhaidi kuliwasilisha kwa Mhe. Chengerwa ili likiridhiwa kiweze kutimiza lengo la kutoa mchango wa kitaaluma wilayani Rufiji.