Habari

Mafunzo yawajenge kusimamia miradi ya Maendeleo – Misungwi

Na Fred Kibano, Mtwara

 

 

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Robert Misungwi ameyafunga rasmi mafunzo ya Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata na kuwataka kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi.

Misungwi ametoa kauli hiyo ya Serikali leo tarehe 30 Novemba, 2023 katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo amewataka watendaji hao kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi kwani Serikali inatoa fedha nyingi hivyo uhamasishaji wa jamii yao kwa kutumia ‘force account’ (kutumia mafundi na vifaa kununua wenyewe) kujenga miradi ya thamani kubwa kwa fedha kidogo ni kipaumbele cha Serikali badala ya kuwategemea wahisani.

“nipende kuwasisitiza kwenda kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwani Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inapeleka fedha nyingi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa vituo vya afya, huduma za maji, madarasa, mabweni na vitu vingine vingi” amesema Misungwi.

Aidha, amewataka watendaji hao kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani, kulinda amani na utulivu, kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi kwenye maeneo yao pamoja na kuwa mfano wa uadilifu kwa wananchi wanaowaongoza.

Kwa upande wake Ibrahim Minja Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa amesema baada ya mafunzo hayo Serikali inategemea watendaji hao wa ngazi ya msingi wataboresha utendaji wao wa kazi hasa katika kuongeza ufanisi kwenye kazi zao pamoja na kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

Naye Bi. Mary Twagabo Afisa Tarafa Newala ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo kwani yamewabadilisa na kuahidi kuwa wabunifu kwa kuwa walivyokuja sivyo wanavyoondoka lakini ametoa ombi kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya msingi kwani huko ndipo Serikali inapoanzia na kuna uhitaji kufanya maboresho zaidi ya kiutendaji.

Back to top button