Habari Tofauti

Wakazi wa vijiji vya Kazania Wilaya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma na Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoro wametakiwa kutunza na kuendeleza Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi

Wakazi wa vijiji vya Kazania Wilaya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma na Melela Wilaya ya Mvomero, Morogoro wametakiwa kutunza na kuendeleza Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ili kukabiliana na ukame.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama alipofanya ziara na kukagua miradi ya kilimo cha mbogamboga kupitia kitalu nyumba, ufugaji wa nyuki na ujenzi wa kisima katika vijiji hivyo inayotekelezwa na EBARR kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.

Amewataka wakazi hao kuwa wamoja kwa kuepuka majungu na fitina hasa katika kipindi cha sasa walichoanza kupata kipato kutokana na uzalishaji wanaoufanya.

Dkt. Mkama amesema kwenye miradi ya kujipatia fedha kwa wananchi wenye ushirikiano kumekuwepo na sintofahamu hali inayosababisha fitina na majungu hivyo kukosekana kwa amani.

“Ndugu zangu nawaomba msiruhusu kabisa kutokea kwa hali hii na endapo kutatokea malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya fedha mntakiwa kufanya uchunguzi na sio kukurupuka kutoa maamuzi kwa kuwa kwenye wengi kuna mengi,“ amesema.

Pia, Dkt. Mkama amewahimiza wananchi kutumia miundombinu inayojengwa ikiwemo visima virefu hatua itakayonusuru mito miwili katika Wilaya ya Mvomero.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wilayani Mvomero wamesema Mradi wa EBARR umekuwa manufaa kwao kwani umewaondolea changamoto mbalimbali.

Wamesema awali walikuwa wanalima mbali na makazi yao ambapo mashamba yao yalikuwa yakivamiwa na tembo, hivyo tangu mradi uanze kutekelezwa wanalima karibu kwa kufanya kilimo cha umwagiliaji.

“Zamani kilimo cha mbogamboga kilikuwa ni kigumu kwani tulikuwa tunategemea maji kutoka kwenye vyanzo vya mito ambayo kwa sasa imekauka lakini baada ya kupata Mradi wa EBARR tumechimbiwa kisima na sasa tunapata maji ya kutosha na kilimo kinaendelea,“ amesema mkazi wa Kata ya Lubungo Wilaya ya Mvomero Bw. Malegesi Chilongo

Hali kadhalika, wameishukuru Serikali kwa kutoa ekari 10 kwa ajili ya wananchi kulima mbogamboga hivyo kuweza kujipatia kipato ambacho kinawasaidia kujikimu.

زر الذهاب إلى الأعلى