Vijana Na Michezo

Balozi wa Tanzania nchini Misri akutana na Uongozi wa Timu ya Yanga na wachezaji

 

Mhe. Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri tarehe 28 Februari, 2024 wakati wa jioni amefika uwanja wa Cairo International Stadium, kuangalia mazoezi ya maandalizi ya timu ya Yanga inayotarajiwa kucheza na timu ya Al Ahly ya Misri siku ya Ijumaa tarehe 01 Machi, 2024.

Timu ya Yanga ambayo imeshafuzu kuingia Robo fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa Barani Afrika imemhakikishia Balozi kupata ushindi mnono katika mechi hiyo.

Aidha, Rais wa Timu ya Yanga, Injinia Hersi Ali Said alimkaribisha Balozi na Maafisa alioambatana nao na aliahidi kufuatilia tiketi za mchezo huo ili Watanzania waliopo Cairo na familia za Maafisa wa ubalozi wafike kwa wingi kushuhudia mchezo huo.

Nae Mhe. Balozi alipata fursa ya kuzungumza na wachezaji na kuwapongeza matokeo mazuri waliyoyapata uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuwataka waitumie ari hiyo hiyo dhidi ya Al-Ahly siku ya Ijumaa kwa sababu tayari wamejaa hofu kufuatia kiwango kikubwa cha mpira kilichoonyeshwa na Timu ya Yanga, lengo ni kuendeleza heshima ya Tanzania katika mashindano hayo Makubwa Barani Afrika.

Back to top button