Habari Tofauti

Tanzania Yashiriki Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (7th Assembly of the Global Environmental Facility, GEF),Vancouver Canada

0:00

Ujumbe wa Tanzania  ukiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Ngelela Maganga unahudhuria Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (7th Assembly of the Global Environmental Facility, GEF) unaofanyika  Vancouver Canada, kuanzia 22 – 26 Agosti, 2023.

Mfuko wa Mazingira wa Dunia ni moja ya mifuko wa Kimataifa inayowezesha shughuli za uhifadhi wa mazingira Duniani hususan katika nchi zinazoendelea.

 Shughuli zinazowezeshwa na mfuko huo  ni pamoja na Hifadhi ya Bioanuai, Mabadiliko ya Tabianchi, Matumizi bora ya Ardhi, Udhibiti wa Taka hatarishi na Kemikali pamoja na Hifadhi ya maji yanayovuka mipaka.

Tanzania ni miongoni mwa  nchi zinazofaidika na mfuko huu katika kuwezesha shughuli za kuhifadhi mazingira nchini.

Katika Mkutano huo Pamoja na mambo mengine, moja ya masuala muhimu yaliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa GEF ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Dunia Kuhifadhi Bioanuai (Global Biodiversity Fund).

Tanzania imepokea na kupongeza azimio la kuanzishwa kwa Mfuko huo. Pamoja na  kuzipongeza nchi zilizotoa ahadi ya kuchangia mfuko huo, Tanzania imeziomba nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuwezesha ukusanyaji wa fedha za kutosha katika mfuko husika. Aidha, Tanzania  imesisitiza mfuko wa Mazingira wa Dunia kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai kupitia Mikakati ya Kitaifa ya Kuhifadhi Bionuai.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi.Mary Maganga umejumuisha Dkt.Richard Muyungi,mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi; Dkt. Thomas Bwana, Mkurugenzi Msaidizi, Hifadhi ya Bioanuai, Ofisi ya Makamu wa Rais;Bw.Charles Faini,Kaimu Balozi, Ubalozi wa Tanzania, Canada pamoja na Bw. Thomas Chali, Afisa Mazingira Mwandamizi, Ofisi ya Makamu wa Rais.

Back to top button