FEDHA ZA CRDB BANK MARATHON KUJENGA KITUO CHA AFYA NA KUPENDEZESHA BUSTANI ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amewapongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu wa kuandaa CRDB Marathon kwa lengo la kuchangia fedha za kusaidia maeneo yenye uhitaji hususani huduma za afya na kupendezesha Miji.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo katika kilele cha msimu wa nne wa Mbio za CRDB Bank Marathon kwa mwaka 2023 zilizoshirikisha washiriki zaidi ya elfu saba kutoka ndani na nje ya nchi katika mabara tofauti zilizofanyika Viwanja vya The Green Oysterbay Jijini Dar es Salaam .
Aidha , Rais Dk.Mwinyi amesema sehemu ya fedha zilizokusanywa Marathon ya msimu huu wa nne kiasi cha shilingi Milioni 100 zimekabidhiwa kwa Wizara ya Afya Zanzibar zitatumika kujenga kituo cha afya cha Mama na Mtoto kwa upande wa Zanzibar itasaidia kuongeza nguvu zaidi katika jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya afya.
Vilevile, fedha zingine zilizopatikana kiasi cha shilingi milioni 20 zimekabidhiwa kwa Baraza la Manispaa ya Mji Mkoa wa Mjini Magharibi zitatumika katika programu ya “Pendezesha Tanzania” ikiwemo kupendezesha Bustani ya Jamhuri, Bustani ya Migombani- Botanic Garden, Bustani ya Tenga-Mnazi mmoja, Bustani ya mbele ya Ikulu Migombani pamoja na njia nne za Michenzani pia itasaidia kuimarisha mazingira ya Miji pamoja na kuendelea kuvutia watalii wanaotembelea Zanzibar.