Habari Tofauti

WAZIRI JAFO ATETA NA WATUMISHI WA OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ushirikiano baina ya viongozi na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais umechangia katika kudumisha Muungano na kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira.

Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao kazi cha Watumishi wa Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma leo Agosti 3, 2023.

Kutokana na hatua hiyo, Dkt. Jafo ameshukuru na kuwapongeza viongozi na watumishi kwa ujumla, kwa kusukuma mbele ajenda ya mazingira kupitia usimamizi wa kanuni na miongozo mbalimbali ya mazingira.

“Ndugu zangu watumishi nitoe pongezi za dhati kwenu kwani mmetumia vyema utaalamu wenu katika kusimamia vizuri hifadhi ya mazingira kupitia kampeni zetu mbalimbali za mazingira,“ amesisitiza.

Pia, Waziri Jafo amewahimzia wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Ofisi hiyo kuendelea kuisimamia vyema ili iendelee kuleta tija kwa wananchi katika maeneo yenye changamoto za mazingira.

Amewahimiza watumishi hao kuishi kwa kupendana na kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kujituma ili kuacha alama nzuri.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amewahimiza watumishi wa ofisi hiyo kuwa wabunifu ili kupata matokeo makubwa katika utekelezaji wa majukumu.

Pamoja na kuwapongeza watumishi hao, pia amewataka waendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwani kwa kufanya hivyo kutachangia katika kusukuma mbele maendeleo.

Pia, ametoa rai kwa watumishi kupitia ubunifu na taalama zao watumie fursa ya teknolojia inayopatikana ili kuboresha mazingra ya kazi na hivyo kufanya utendaji wa kazi kuwa rahisi na wenye tija.

“Kama mnavyojua sasa hivi tumeshaanza mwaka mpya wa fedha na hivyo nina matarajio makubwa sana kutoka kwenu watumishi kuona mnafanya kazi kwa bidii na hivyo Ofisi inapata matokeo mazuri,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Back to top button