Waziri apongeza watumishi wa Afya Maswa kwa kutoa huduma nzuri
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu yenye lengo la kufuatilia utoaji wa huduma za afya katika ngazi mbalimbali na kuhimiza watumishi wa afya kuzingatia weredi, maadili na viapo vyao katika utoaji wa huduma za afya.
Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo wakati akiongea na watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa wakati akitembelea na kukagua huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ambapo amewapongeza watumishi kwa kutoa huduma nzuri.
Amesema serikali inatambua changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya, hivyo amewataka watumishi kuwahudumia wananchi kwa weredi wakati serikali ikiendelea kuongeza watumishi wa sekta hiyo na kuboresha miundombinu yote ya afya kwa kuimalisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Pia Waziri wa Afya amesema serikali imeweka Mazingira mazuri kwa watumishi ili waweze kufanya kazi zao vizuri kwa kuwa serikali imetenga bajeti kubwa ambapo Wilaya ya Maswa imeongezewa bajeti kutoka Shilingi milioni 244 hadi shilingi bilioni 1.9 katika sekta ya afya.
Pia Mhe. Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kuboresha huduma za afya katika utoaji wa chanjo za polio, UVIKO-19 pamoja na chanjo zingine ambazo zimepunguza sana vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Aidha Waziri wa Afya ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kuajiri watumishi wa afya 65 kwa mkataba kupitia Fedha za mapato ya ndani na amewataka waendelee kufanya hivyo ili kuwasaidia wataalamu katika utoaji wa huduma za afya kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi wa Maswa.
Vilevile Mhe. Mwalimu amewashukuru wadau wa maendeleo Mkapa Foundation na AMREF kwa kuajiri watumishi 36 ambao wameisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa watumishi sambamba na hilo ametoa kongole kwa Wilaya kwa kuwa Hospitali ya wilaya, Zahanati na vituo vingi vya afya vimefungwa mfumo wa GOT HOMIS ambao utasaidia ukusanyaji wa mapato.
Akiwa wilayani Maswa Waziri wa Afya ametembelea na kukagua jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa kuona huduma zinavyotolewa na wataalamu, ametembelea Chuo cha Maafisa tabibu na kuzungumza na watumishi pamoja na wanachuo, ametembelea jengo la watoto njiti na kuona namna ambavyo wanapatiwa huduma pamoja na Zahanati ya barikiwa iliyoko Kata ya Shanwa.