Habari Tofauti

MKURUGENZI WA MAZINGIRA OFISI YA MAKAMU WA RAIS ATETA NA WADAU PAMOJA NA WABIA WA MAENDELEO

0:00

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amekutana na kufanya mazungumzo na wadau na wabia mbalimbali wa maendeleo ikiwa ni mwendelezo wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mazingira nchini.

Wadau na wabia hao wa Maendeleo ambao wametembelea Ofisi ya Makamu wa Rais, Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA), Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS) na Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza, Tanzania.

Kwa upande wa Shirika la KOICA, ujumbe huo ulieleza utayari wa Shirika katika kuwekeza katika miradi ya maendeleo uendelevu wa nishati jadidifu kupitia ufadhili wa Green Climate Fund -GCF.

Ujumbe huo uliieleza Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais hatua mbalimbali ilizofikia ikiwemo uaandaji wa andiko la mradi katika hatua za awali kufanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuweza kubaini na kukubaliana maeneo ya ushirikiano.

Aidha kuhusu IFAD, ujio wa watalaamu hao ulilenga katika kuzungumzia kuhusu maandalizi ya mfuko huo kuelekea Mkutano wa Jukwaa la Kilimo unaotarajia kufanyika Tanzania mwezi Septemba mwaka huu.

Kwa upande wa UNOPS, Ofisi hiyo ilieleza madhumuni ya ziara hiyo ni kuonesha nia ya kuendelea kufanya kazi na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia miradi wa kukabiliana na Athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Bahari ikiwemo ujenzi wa ukuta katika Barabara ya Baraka Obama pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji katika Manispaa ya Ilala.

Back to top button