Jamii imetakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika hifadhi ya mazingira

Jamii imetakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika hifadhi ya mazingira kwa kupanda miti na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.
Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Bw. Abdalla Shaibu Kaim wakati wa ukaguzi na uzinduzi wa miradi wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza mara baada ya kupanda mti wa kumbukumbu katika kitalu kilichopo Rongai wilayani humo kinachomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kaim amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi hiyo wa kuhifadhi mazingira.
Pia, ametoa wito wa kuendelea kuelimisha wananchi wafahamu umuhimu wa kupanda miti na kuepuka kukata miti kiholela bali kuipanda na kuitunza ili ikue hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunawapongeza TFS kwa kuunga mkono ujumbe wa Mwenge wa Uhuru ambao unasisitiza uhifadhi wa mazingira na tunatambua kazi hii kubwa ya kizalendo na utekelezaji wa agizo la Serikali la kuhakikisha tunakuwa na programu za upandaji miti kwani sote tunatambua athari za mabadiliko ya tabianchi zinaathiri uchumni na uhai wa viumbe,” amesisitiza Kaim.
Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Kilimanjaro pia uliwasili katika Wilaya ya Siha ambapo kiongozi huyo aliendelea kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira ambapo alipanda mti katika Shule ya Sekondari Nuru iliyopo Kata ya Makiwaru.
Mwenge wa Uhuru unaendelea kukimbizwa katika mikoa mbalimbali nchini ambapo ujumbe wa mwaka 2023 ni “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.