Vijana Na Michezo

Makamu wa Tanzania ashuhudia Tamasha la Bunge Grand Bonanza

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni muda muafaka wa kupinga kwa nguvu zote tabiabwete ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wabunge pamoja na Watumishi wa Bunge mara baada ya kumalizika kwa Tamasha la Bunge Grand Bonanza lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya John Merlin Jijini Dodoma leo tarehe 24 Juni 2023. Amesema watanzania wengi hususan wanaoishi mijini wanakabiliwa na hali ya uzito uliozidi na viribatumbo na baadhi ikiwemo vijana kupoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na mtindo wa maisha, ulaji usiofaa na kutofanya mazoezi.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa Bunge kufanya semina au mjadala utakaolenga kuibua mapendekezo na mikakati mipya ikiwemo aina za uwekezaji endelevu, kutambua na kulea vipaji vitakavyowezesha michezo ambayo Tanzania inaipa kipaumbele ili kushinda katika mashindano ya kikanda na kimataifa katika kipindi kifupi.

Aidha amewahimiza Wabunge wa kila mkoa kwa umoja wao kuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kulea timu za michezo katika mikoa au majimbo hususani timu za wanawake, vijana wa shule za msingi na sekondari na watu wenye ulemavu. Pia ametoa wito wa ushirikiano baina ya Bunge na Serikali kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanalindwa na hayabadilishiwi matumizi. Vilevile amesema ulinzi wa maeneo ya michezo unapswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti kuzunguka viwanja vya michezo ili kuhakikisha upatikanaji wa hewa safi wakati wananchi wanapofanya mazoezi au kushiriki mashindano mbalimbali.

Makamu wa Rais amesema hivi sasa michezo imebainika kuwa na nafasi kubwa katika kukuza uchumi duniani kote ambapo ujenzi wa miundombinu ya michezo, kushamiri kwa sekta ndogo ya burudani na uzalishaji wa vifaa vya michezo ni chanzo kikubwa cha ajira na mapato.

Bunge Grand Bonanza limehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa , Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela na wawakilishi wa Benki hiyo pamoja na Watumishi wa Bunge. Tamasha hilo limefanyika kwa ushirikiano na Benki ya CRDB ambapo limeenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Tupende Michezo, Tujenge Taifa letu”.

Back to top button