Habari Tofauti

WAKUU WA MIKOA DHIBITINI MAAMBUKIZI YA MALARIA

Ahmed Hassan

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha Maambukizi ya Malaria ianze kusimamia utekelezaji wa afua za ugonjwa huo ili kupunguza viwango hivyo.

Amesema kuwa lengo la Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutokomeza maambuzi ya ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 “Upatikanaji wa afua za kinga kama vyandarua vyenye dawa na upatikanaji wa vitendanishi na dawa za malaria utasaidia sana kupungua kwa idadi ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na Malaria hapa nchini”

Ametoa wito huo leo Jumanne (Aprili 25, 2023) wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2023 ambapo Kitaifa yamefanyika Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonesha mikoa inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria ni Tabora una asilimia 23, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara una asilimia 15.

“Kwa upande mwingine, nimeelezwa kuwa mikoa 9 ina kiwango cha maambukizi chini ya asilimia moja nayo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Iringa, Dar es salaam na Mwanza. Kwa namna ya pekee kabisa ninaipongeza sana mikoa yote iliyofanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria”.

Ameongeza kuwa takwimu zilizopo zinaonesha kuendelea kupungua kwa maambukizi ya Malaria mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022. “nitoe wito kwa kuendelea kuongeza nguvu katika mapambano ya kutokomeza Malaria”.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya kufanya kampeni ya kutosha katika kuhamasisha matumizi ya vyandarua vya kisasa hadi maendeo ya vijijini.

“Naipongeza Wizara ya Afya kwa dhamira ya dhati katika mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania. Hivi sasa, zaidi ya 98% ya kesi za malaria zinathibitiwa, kesi za malaria zilizothibitiwa kwa mwaka zinaonesha kati ya kila watu 1,000 zilipungua kutoka 106 mwaka 2020 hadi 76 mwaka 2021 na zaidi hadi 58 mwaka 2022”.

Back to top button