Habari Tofauti

MISS KIZIWI DUNIA NA WAGUMBA KUNUFAIKA NA MFUKO WA HISANI MERCK (MERCK FOUNDATION)

0:00

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya MERCK FOUNDATION Seneta Dkt. Rasha Kelej amesema Taasisi hiyo ipo tayari kumlipia ada mshindi wa dunia mwaka 2022 wa mashindano ya urembo wa wasichana wasioona Bi. Khadija Kanyama ili kuendeleza maono yake ya kuwa mtaalamu wa ustawi wa jamii kwenye eneo la makundi maalum.

Dkt. Rasha ameyasema hayo Aprili 03, 2023 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo, Profesa Frank Stangenberg katika Makao ya kulea watoto Kurasini Dar es salaam na kuzungumza na watoto wanaolelewa kwenye Makao hayo, baadhi ya viongozi wa Chama cha wagumba na baadhi ya vikundi vya Wanawake wajasiriamali, akiwa katika ziara ya siku mbili nchini kwa lengo la kukutana na wanufaika wa Taasisi hiyo.

Aidha, ameahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuwawezesha kiuchumi wanawake hususani wagumba kupitia mradi uitwao “More than a Mother”.

“Wagumba ni kundi muhimu kwani mwanamke ni zaidi ya kuwa mama, kuwa wagumba haimaanishi nyie hamna mchango wowote kwenye Jamii” amesema Dkt Rasha.

Mwenyekiti wa Bodi Profesa Frank Stangenberg amesema taasisi hiyo iko tayari kufanya kazi na Tanzania katika maendeleo ya wanawake na watu wenye uhitaji maalum.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Gwajima ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kusaidia Makundi Maalum nchini.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha idadi kubwa ya Wanawake wote bila kujali tofauti zao wanainuliwa katika sekta mbalimbali.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Wizara kwa ushirikiano na Mkoa wa Dar es Salaam ina mpango wa kutafuta rasilimali ili kujenga Makao ya Kisasa ya Watoto eneo la Kigamboni ambapo, kutakuwa na huduma za kutambua na kuendeleza vipaji vya watoto Yatima na wote watakaobainiwa kuhitaji huduma za makao hayo.

Maeneo mengine ambayo viongozi hao wamekubaliana yataainishwa kwenye andiko la makubaliano rasmi baada ya itifaki zote kukamilika.

Taasisi ya MERCK FOUNDATION inajishughulisha na kuboresha afya na ustawi wa watu pamoja na kuendeleza maisha yao.

Back to top button