Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi wa umma kuwajibikaji kwa kero na changamoto wanazowasilishiwa na mfumo wa Sema Na Rais (SNR) .Amesema wapo baadhi ya viongozi wasiotaka kutatua changamoto hizo kwa vile hawaoni umuhimu wake na akawaonya atawachukulia hatua . Dk.Mwinyi halikadhalika amebainisha kupitia mfumo huo kuna utambuzi wa kitakwimu kujua kiongozi au taasisi zisizofanya vizuri na sasa wakati umefika kila mmoja aone umuhimu wa kuwajibika.
Rais Dk.Mwinyi ameyaeleza hayo leo katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport kwenye kikao kazi cha maadhimisho ya miaka miwili tangu kitengo cha Sema na Rais Mwinyi (SNR) kilipoasisiwa .Kitengo hicho kipo chini ya Afisi ya Rais Ikulu.
Aidha, Rais Dk.Mwinyi akizungumzia mafanikio ya mfumo wa SNR kwa kipindi hicho cha miaka miwili alisema mfumo huo umeleta tija kwa wananchi ambao changamoto zao zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa na mfumo ataendelea kuusimamia vema.
Alizungumzia pia suala la taarifa za ubadhirifu wa mali za umma na akaonya asitokee Kiongozi yeyote kuwatisha wanaowasilisha kero au changamoto kupitia mfumo wa SNR na akaahidi hatua zitachukuliwa dhidi ya kiongozi huyo. Ameahidi mtoa taarifa atalindwa na kuwaambia maafisa wa SNR wafanye kazi zao bila woga.
Vilevile, Rais Dk.Mwinyi alieleza kuthamini uhuru wa Mahakama na Serikali itayafikisha mbele ya haki matatizo yatakayopelekwa na SNR Mahakamani kwa Jaji Mkuu ayashughulikie na kuondoa kasoro zinazojitokeza .Katika msingi wa utawala bora Mheshimiwa Rais alibainisha Serikali haina haki kuingilia mhimili wa Mahakama ila ina wajibu kuwasilisha changamoto wazishughulikie.