Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzisha Kituo cha Nyaraka za Muungano
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameileza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuanzisha kituo cha Kumbukumbu na Nyaraka za Muungano ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za Muungano.
Alisema hayo jana, jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa Kamati hiyo.
Dkt. Jafo amesema Mungano wa Tanganyika na Zanzibar umeendelea kuimarika kutokana na upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi na hivyo kuufanya uwe wa kipekee duniani.
Amesema Serikali itafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Pamoja na yale masuala 22 ya Muungano kwa mujibu wa Katiba wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika ipasavyo.
“Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia wataalamu wetu itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano na faida zake kwa jamii kupitia vyombo vya habari na maadhimisho mbalimbali. Ili kuboresha utoaji elimu kwa umma, Ofisi imeandaa Kitabu cha Historia ya Muungano kitakachotumika kuelimisha umma kuhusu faida za Muungano kiuchumi, kijamii na kiutamaduni,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Joseph Mhagama pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wamepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa taarifa nzuri.
Wamesema kuna umuhimu wa kutoa ufafanuzi kuhusu hoja za Muungano zilizotatuliwa ili wananchi wapate uelewa kuhusu mambo gani yaliyopata ufumbuzi kwa pande zote mbili.