Habari
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imejipanga kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi mwishoni mwa mwezi wa tatu mwaka huu ili kuendeleza mahusiano yaliyopo baina ya Tanzania na Malawi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokutana na Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Hamphrey Polepole alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona ni namna gani Taasisi hiyo itakavyotoa huduma ya matibabu ya moyo nchini humo.
Dkt. Kisenge alisema JKCI imekuwa ikiendelea vizuri tangu ilipoanzishwa mwaka 2015 kwa kutoa huduma za tiba na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa hapa nchini pamoja na wagonjwa kutoka nchi za Comoro, Malawi, Zimbambwe, Ethiopia, Kenya, Rwando, Burundi, Congo pamoja na nchi nyingine za nje ya Afrika.
Dkt. Kisenge alisema Tanzania na Malawi imekuwa na mahusiano mazuri kwani JKCI imekuwa ikiwapokea wagonjwa kutoka nchini humo kwa ajili ya kuwahudumia hivyo basi umefika wakati kwa Taasisi hiyo kwenda kutoa huduma ya matibabu nchini Malawi.
Aidha Dkt. Kisenge alimshukuru Mhe. Polepole kwa kutenga muda wake na kutembelea Taasisi hiyo ili kwa pamoja waweze kushirikiana kupeleka huduma za matibabu na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wa moyo waliopo nchini Malawi.
“Nawahakikishia wananchi wa Malawi kwa kufika hapa kwetu kupata huduma za matibabu watakuwa wamechagua sehemu sahihi ambayo itawatatulia matatizo ya magonjwa ya moyo yanayowakabili kwa gharama nafuu tofauti na wakienda sehemu nyingine duniani kutafuta huduma hizi”, alisema Dkt. Kisenge
Naye Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Hamphrey Polepole alisema uhusiano wa kimashirikiano ambao amekuwa akiupata kutoka JKCI umempa motisha wa kuona umuhimu wa kufika katika Taasisi hiyo ili kwa pamoja waweze kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha mahusiano ya afya upande wa matibabu ya moyo kati ya Tanzania na Malawi.
“Kazi yetu ubalozini ni kufanyia kazi mahusiano ya Tanzania na Malawi tukiangazia sera ya mambo ya nje, kwetu sisi tumeona Tanzania imefanikiwa kujenga ubobezi kwenye sekta ya afya katika maeneo ya tiba ya moyo, tiba ya mifupa na tiba ya figo hivyo kuanza kushirikiana na Taasisi hii kusogeza huduma za matibabu ya moyo nchini Malawi”, alisema Mhe. Polepole.
Mhe. Polepole alisema kwa sasa wananchi wa Malawi wanafuata huduma za matibabu ya moyo nchini Afrika ya Kusini na India nchi ambazo zipo mbali kidogo na nchi ya Malawi lakini pia gharama zake ni kubwa tofauti na wagonjwa hao wangetibiwa Tanzania.
“Tumejipanga kwa kuanzia tutawakaribisha nchini Malawi mfanye kambi ya matibabu ya moyo nchini humo ili wananchi wapate huduma ya matibabu haya wakiwa nchini mwao na baada ya hapo waje kutibiwa nchini kwetu kama ambavyo baadhi ya wananchi wa Malawi wanakuja kutibiwa hapana”, alisema Mhe. Polepole.