Habari

Dkt. Mahera: Simamieni utoaji wa huduma za malezi ya watoto 

Fred Kibano - Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya,  Dkt. Wilson Mahera amewaasa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wa Wizara za kisekta kuboresha na kusimamia utoaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto nchini.

Akifunga mafunzo hayo ya Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto leo Julai, Mosi, 2023 jijini Dodoma, Dkt. Mahera amesema serikali inatambua umuhimu wa kuwajengea uwezo wataalam ambao  watachochea uwekezaji mkubwa zaidi kwenye malezi na makuzi bora  ya watoto wa Tanzania.

Aidha, amewataka Maafisa hao kwenda kuutumia ujuzi walioupata kwenye maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi nane wanapatiwa huduma bora za malezi, lishe, ujifunzaji wa awali na usalama wao kwa ustawi wa Taifa ikiwa ni pamoja na wao wenyewe kuonyesha utofauti walivyokuwa hapo awali na baada ya kupata mafunzo hayo.

“Napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa wataalam mliopata  mafunzo haya mkatumie elimu mliyoipata kwenye maeneo mnayofanyia kazi pia mkawe mabalozi wa kuhakikisha watoto wadogo  wenye umri wa miaka 0-8 wanapatiwa huduma za malezi jumuishi ikiwemo Afya bora, Lishe Bora, Malezi yenye Mwitikio, Ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama” amesisitiza Dkt. Mahera.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Haki na Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku amesema Serikali imekuja na Programu mahususi ya kuwatengeneza watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8 kwa kuzingatia maeneo manne ya afya, lishe, ujifunzaji wa mtoto na makuzi ya mtoto mwenyewe kwa kuwa ndio eneo ambalo asilimia 90 ya ubongo wa binadamu unatengenezwa kupata watu wanaofikiri na hivyo uwekezaji huo utalisaidia Taifa katika nyanja mbalimbali hapo baade.

Akitoa neno la shukrani Martin Chuwa Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Maendeo ya Jamii Mikoa Tanzania Bara amesema mafunzo hayo yatasaidia katika kukabiliana na changamoto za jamii ambazo wanakutana nazo lakini pia kuboresha mafunzo katika ngazi za Mikoa na Halmashauri.

Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, shirika la ‘’Children in Crossfire’’ pamoja na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari vinara wa MMMAM Tanzania kupitia Mradi wa Mtoto Kwanza washiriki wakiwa Maafisa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa  Maendeleo ya Jamii wa Mikoa Mikoa 16.

Back to top button