Waziri Mkuu atembela bandari ya Tanga
Leo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembela bandari ya Tanga na kukagua uboreshaji mkubwa wa miundombinu katika bandari hiyo uliohusisha ujenzi wa gati ambao umefikia asilimia 99% pamoja na uongezaji wa kina cha bandari ili kuruhusu meli kutia nanga na kugeuza kwa urahisi.
Uboreshaji huo ambao umetumia Shilingi Bilioni 429, umewezesha kujengwa kwa gati yenye urefu wa mita 450, kuongeza njia ya kupitishia meli yenye urefu wa kilomita 1.7 na upana wa mita 700.
Ujenzi huo utawezesha meli kutia nanga katika bandari hiyo na kupakua mizigo kwa urahisi tofauti na awali ambapo mizigo ilishushwa mbali na kupakiwa katika Matishari ili kufikishwa bandarini.
Akizungumzia maboresho hayo Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na uboreshaji huo na kusema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufanya maboresho ya bandari nchini yanaendelea kukamilika.